Kwa kuwa siyo watu wengi hufikia hatua hii,
unapopata taarifa rasmi kuwa umeitwa kwenye usaili wa kazi uliyoiomba, ni jambo
la kujivunia. Kushindana na kundi la watu wengi waliohitaji kazi hiyo na
hawakuitwa, siyo jambo dogo.
Hata hivyo, ni vizuri kutambua kuwa usaili wa
kazi sio kupata kazi. Wapo watu waliowahi kuitwa kwenye usaili mara nyingi
lakini hawakupata kazi. Makala haya yanakupa dondoo chache za kukusaidia
kufanya usaili kwa mafanikio.
Leo tutajitahidi kujadili mambo halisi ya
kukuwezesha kushinda usaili na kupata kazi.
ELEWA
MALENGO YA USAILI
Kwa kawaida, usaili ni mahojiano kati ya
mwombaji wa kazi na mwajiri kwa lengo la kutathmini uwezo wa kikazi alionao
mwombaji. Mahojiano haya aghalabu hufanyika kwa mazungumzo au maandishi katika
chumba au eneo lolote linaloteuliwa na mwajiri kwa kazi hiyo na Huwezi
kujiandaa vizuri na usaili bila kuelewa malengo ya usaili.
Hata hivyo, si lazima mwajiri
awepo kwenye usaili. Wakati mwingine mwajiri hukasimu mamlaka yake kwa watu
anaowaamini kwa kazi hiyo. Jopo hilo hufanya kazi ya kukusanya taarifa
zinazotumika kufanya maamuzi ya ikiwa mwombaji wa kazi anaweza kuajiriwa ama
la. Kwa muktadha huu, kinachoamuliwa na jopo hilo halali, kinawakilisha matakwa
halisi ya mwajiri.
Jambo la msingi kuzingatia ni kuwa
unapokwenda kwenye usaili wa kazi, una wajibu wa kuthibitisha kuwa unafaa kwa
nafasi unayoomba. Hilo litawezekana ikiwa utaonyesha namna uwezo wako, maarifa
yako, na ujuzi ulionao yanavyowazidi watu wengine wanaoshindana kupata nafasi
hiyo unayoiomba.
FANYA
UTAFITI WA TAASISI
Maandalizi yanaanza kwa kufanya utafiti wa
taasisi unayotarajia ikupe kazi. Uelewa wa taasisi ni muhimu kwa sababu maswali
mengi utakayokabiliana nayo siku ya usaili, kwa kiasi kikubwa yanategemea namna
unavyoielewa taasisi unayotaka ikuajiri.
Katika kufanya utafiti,
unahitaji kuelewa historia ya taasisi, dira na malengo yake, mfumo wa utendaji
wake, uongozi wake, walengwa katika huduma zake na mambo kama hayo. Uelewa wa
kina maeneo hayo utakusaidia kujibu kwa ufasaha maswali yanayoweza kujitokeza
siku ya usaili.
Ili uweze kufanya utafiti, unahitaji
kufuatilia tovuti ya taasisi hiyo, kurasa za taasisi katika mitandao ya kijamii
na machapisho mbalimbali yanayopatikana mtandaoni. Pia, unaweza kuwasiliana na
watu wanaoifahamu taasisi husika na kujaribu kupata taarifa zitakazokusaidia.
JIANDAE
KISAIKOLOJIA
Unahitaji kuiandaa akili yako kwa ajili ya
siku ya usaili. Amini kuwa upo uwezekano mkubwa wa kupata kazi uliyoitiwa.
Unapokuwa na mawazo chanya, ni rahisi kujenga hali ya kujiamini itakayokusaidia
kufanya vizuri zaidi kwenye usaili.
Ni makosa kwenda kwenye usaili hali ukiamini
hutapata kazi. Hisia kuwa unatimiza mradi tu, zitakuondolea nguvu za kufanya
vizuri.
Hata kama ni kweli mara
nyingi umeitwa kwenye usaili wa kazi na hukufanikiwa, amini kuwa safari hii
utapata kazi. Imani inajenga kujiamini, kujiamini kunajenga ujasiri.
Kama una wasiwasi na kujiamini kwako, tafuta
watu wenye maneno ya kuinua moyo wakusaidie. Soma maandiko yanayokuinua moyo.
Kwa kusikia na kusoma maneno yanayokujenga, utaimarika kisaikolojia na kuwa
jasiri zaidi.
Sambamba na hilo, epuka kuongea na watu
wanaokukatisha tamaa wanaokuonyesha kuwa hutapata kazi. Ukijiruhusu kukutana na
watu wa namna hii, utaishia kuvunjika moyo na utashindwa kufanya vizuri.
HAKIKI
MUDA NA MAHALI PA USAILI
Kosa kubwa unaloweza kufanya
siku ya usaili ni kuchelewa. Unaweza kuchelewa kwa sababu nyingi.
Moja, kutokukumbuka muda halisi wa kuanza kwa
usaili. Ni rahisi kuchelewa unapokuwa huna hakika na muda halisi wa kuanza
usaili.
Pili, unaweza kuchelewa kwa sababu huna uhakika na
mahali patakapofanyikia usaili. Kubahatisha namna ya kufika eneo la usaili siku
ya usaili, unajiweka kwenye hatari ya kuchelewa, na wakati mwingine, hata
kushindwa kufika. Tafuta ramani ya eneo mapema, jiridhishe na namna
utakavyoweza kufika. Hiyo itakusaidia kukadiria muda wa kuondoka nyumbani au
mahali ulikofikia ili uweze kuwahi usaili.
Ikiwa unahitaji kusafiri
umbali mrefu, usisubiri siku ya mwisho kuanza safari. Fika mapema kwenye eneo
lililo karibu na mahali patakapofanyikia usaili, ili upate muda wa kupumzika na
kutulia kifikra.
MAANDALIZI
YA MWISHO
Unahitaji kuonekana nadhifu siku ya usaili.
Ingawa hulazimiki kuvaa mavazi ya gharama na ya namna fulani, hata hivyo
unahitaji kuvaa nguo za heshima. Epuka kuvaa nguo zitakazotoa picha ya mtu
asiye rasmi. Mavazi mafupi, yanayobana, milegezo, mitindo inayozidi kiasi na
mavazi yenye maandishi hayawezi kuwa chaguo sahihi.
Andaa nyaraka muhimu kama
vyeti halisi, cheti cha kuzaliwa, kitambulisho, barua ya kuitwa kwenye usaili
kama umepewa na nyaraka nyingine kama ulivyoelekezwa. Ingawa nyaraka hizi
zinaweza zisihitajike, lakini unapokuwa nazo unakuwa na utulivu wa nafsi na
akili.
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv