Wengi hawamjui Valentine Strasser ambaye aliwahi
kuwa rais wa nchi ya Sierra Leone kati ya Aprili 29, 1992 hadi Januari 16
, 1996 akiwa ndiye amiri jeshi mkuu na kiongozi wa ngazi ya juu kwenye taifa
hilo lililopo kaskazini-magharibi mwa bara la Afrika.Wakati akiingia madarakani
aliweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mdogo zaidi, yaani akiwa na chini
ya miaka 25.
Aprili 29, 1992, Strasser akiwa kijana
mwanajeshi mwenye cheo cha kapteni, akiwa na umri wa miaka 25, aliwaongoza
wanajeshi wenzake kuvamia Ikulu ya Sierra Leone, walimkuta rais amejificha
ndani ya kabati lililopo kwenye chumba cha kuogea, kisha wakamteka Rais Joseph
Saidu Momoh na wakamlazimisha kukimbia, naye akatorokea Conakry, Guinea.
Strasser
alichukua madaraka ya nchi hiyo siku tatu tangu ashehereke sikukuu yake ya
kuzaliwa.
Baada ya Momoh kutorokea Conakry, Strasser
alijitangaza kuwa Rais wa Sierra Leone. Aliwaongoza vijana wenzake sita
waliofanikisha mapinduzi hayo na kuunda serikali ya mpito waliyoipa jina la National Provisional Ruling Council (NPRC).
Maisha yakabadilika, alishakuwa mkuu wa nchi,
kwa hiyo hakutaka kuishi kwenye nyoyo za Wasierra Leone. Hakulipa malimbikizo
ya mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma.
Alifuja almasi ya Sierra Leone, kwa vile jina
lake ni Valentine, basi sikukuu ya Valentine’s Day akaifanya kuwa sherehe ya
kitaifa yenye mapumziko huku sherehe kubwa ikiandaliwa ikulu ya nchi hiyo.
Strasser alikuwa na mbwembwe nyingi, mwaka 1993
katika mkutano wa wakuu wa serikali katika nchi za Jumuiya ya Madola,
uliofanyika Limassol, Cyprus, alitinga kwa mbwembwe akiwa amevaa suruali ya
jeans na fulana yenye maandishi Sunny Days in Cyprus (Siku za Jua Kali Cyprus).
Alikuwa
mtu wa starehe, vurugu nyingi kwa wanawake, aliua watu wasio na hatia.
Strasser alisahau kuwa ipo siku uongozi
hautakuwa kwenye mikono yake, na ambacho kinaweza kumfaa ni kuishi ndani ya
mioyo ya watu ili wamtetee na kumpigania baadaye. Januari 16, 1996, Strasser
alipinduliwa na msaidizi wake, Brigedia Jenerali Julius Maada Bio.
Strasser akakimbilia Uingereza, akajiunga na
Chuo Kikuu cha Warwick, kilichopo mjini Coventry, akaanza masomo ya sheria,
akasema anataka awe wakili ili awatetee Waafrika.
Mwaka
mmoja wa masomo, Strasser aliishiwa fedha, akaacha chuo.
Maisha Uingereza yakawa magumu, akakimbilia
Gambia nako kukawa pagumu, mwisho akarudi Sierra Leone, mjini Grafton,
mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Freetown.
Kazi ya kwanza ambayo Strasser aliifanya,
ikawa kuanzisha kichuo kidogo cha kufundisha kompyuta na teknolojia ya
habari na mawasiliano (Tehama). Maisha ya chuo yakamshinda.
Baada ya kila kitu kwenda kombo, Strasser
alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi na kuishi kwenye banda la uani.
raisi huyo kwa sasa |
Hata sasa, akiwa na umri wa miaka 49, anakunywa pombe za kienyeji mtaani.
Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi
mstaafu. Strasser anaishi kama mtu wa kawaida tu mtaani. Mlevi na hakuna
anayemjali.
Hana mtu wa kumtetea wala kumpigania kwa sababu
hakuishi kwenye nyoyo za watu. Strasser ndiye mkuu wa nchi wa zamani, anayeishi
kimaskini kuliko wakuu wote wa nchi duniani.
Ukiwa
kiongozi na kugeuka kituko kama Strasser inawezekana kabisa.
Siyo vizuri kuishi vibaya na watu wasikupende,
akija mtawala ambaye hatakutambua kama mkuu uliyepita, unaweza kuishi maisha ya
hovyo kama ombaomba mtaani au kuwa mnywa gongo uliyeshindikana.
Sasa viongozi wote duniani watambue kwamba uongozi
ni dhamana, wafanye kazi kwa kujituma na wataishi mioyoni mwa wananchi
waliowaongoza milele. Kuna viongozi wengi
waliofanya mema na bado wanaenziwa mpaka sasa kama Julius Nyerere na Nelson
Mandela, wako wengi hawa ni baadhi tu ya viongozi walioweka mbele maslahi ya
wananchi wao na watakumbukwa milele. global
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv