Barua ya kuomba kazi ni waraka ambao mara nyingi husomwa kabla ya waraka mwingine wowote unaoambatanishwa katika kuomba kazi.

Ni vyema barua hii ikaandaliwa kwa umakini, huku ikijaribu kugusa kwa ufupi mambo yaliyoonekana kwenye wasifu binafsi. Tutazame mambo sita makubwa ya kuzingatia unapoandika barua ya kuomba ajira.
Kanuni za uandishi wa barua
Inafahamika kuwa barua rasmi ya kiofisi hufuata kanuni kadhaa. Moja ni kuwapo kwa anuani mbili. Juu kulia, kuonekana anuani ya mwandikaji isiyotanguliwa na jina na chini kidogo ya anuani hiyo upande wa kushoto mwa barua, huonekana anuani ya mwandikiwa.
Pili, huwa na tarehe chini ya anuani ya mwandikaji au juu ya anuani ya mwandikiwa. Tatu, huwa na kichwa cha habari kinachoonyesha lengo, kikitanguliwa na salamu rasmi kama Ndugu, Dear Sir/Madam.
TATU Huna sababu ya kutaja jina la mwenye kupokea maombi hayo hata kama unamfahamu kwa jina lake. Barua yako inaelekezwa kwa ofisi, siyo mtu.
Nne, barua huwa na maelezo yanayofafanua lengo la barua na mwisho huonekana saini na jina la mwandikaji. Fuata kanuni hizo.
Kichwa cha habari kitaje kazi inayoombwa
Hakikisha kichwa cha habari kinajitosheleza na kinaeleza wazi wazi kitu gani unachokitaka. Chagua maneno kwa umakini mkubwa kwa sababu wapo wasomaji huishia kusoma kichwa cha habari na kufanya maamuzi.
Mfano,
‘YAH: KUOMBA KAZI YA MHASIBU MSAIDIZI
Hapo msomaji anaelewa kwa uwazi barua inahusu nini. Epuka kutumia maneno yasiyoeleweka au yasiyo rasmi.
Onyesha ulikopata habari za kazi unayoomba
Baada ya kuridhika na kichwa cha habari, ni muhimu sentensi inayoanza chini yake ifanye rejea kwenye tarehe ya tangazo la kazi unayoomba, namba ya kumbukumbu ya tangazo (kama ipo) na mahali tangazo hilo lilipoonekana.
Mfano, “Rejea tangazo la nafasi ya kazi lenye kumbukumbu namba XXX katika gazeti la Mwananchi la tarehe 25 Oktoba 2016.”
Wengine wanapenda kuandika sentensi kama, “Kichwa habari hapo juu chahusika”. Haya ni mazoea tu lakini hayana sababu ya msingi.
Sema wazi kuwa unaomba kazi
Baada ya kusema ulikopata habari za kazi unayoomba, tumia sentensi inayofuata kueleza nia yako ya kuomba kazi hiyo. Kumbuka msomaji wa barua hana muda wa kusoma maelezo yako mengi, ni muhimu kuandika kila kitu kwa kifupi na kwa uwazi.
Mfano, “Ninaandika barua hii kuomba kazi ya Uhasibu katika kampuni/shirika/taasisi yako kama ilivyoelekezwa kwenye tangazo nililolitaja.”
Oanisha majukumu ya kazi na ujuzi ulionao
Anza aya mpya kwa kumshawishi msomaji kuwa unaweza kumudu majukumu yaliyotajwa kwenye tangazo lake. Ili kufanya hivyo, una kazi ya kuoanisha ujuzi, sifa za kitaaluma na uzoefu ulionao na mahitaji ya kazi.
Kabla hujaandika barua, jaribu kuainisha pembeni namna unavyoweza kukidhi sifa zinazotajwa kwenye tangazo na barua yako ionyeshe hivyo.
Mfano, “Ninao uwezo wa kutunza kumbukumbu sahihi za mahesabu ya kampuni yako, kwa sababu, mbali ya kusomea Cheti cha Uhasibu katika Chuo cha Uhasibu Singida, nina uzoefu wa kujitolea kwa miezi 13 nikifanya kazi za uhasibu katika kampuni XXX. Kadhalika, nimepata mafunzo ya kutunza fedha kwa njia ya mtandao hivyo ninaweza kumudu majukumu hayo ipasavyo.”
Vile vile, hakikisha barua yako inajibu kila jukumu lililoonyeshwa kwenye tangazo la kazi. Hata hivyo, hiyo haimaanishi uandike mambo mengi.
 
Hitimisha kwa uungwana na ufasaha
Ni vyema kuhitimisha barua yako kwa kuonyesha unavyofaa kwa kazi unayoiomba. Uchaguzi makini wa maneno kutakupa alama za ziada ikiwa itaonyesha unavyojua kuwasiliana vizuri.
Kwa mfano, unaweza kusema unatanguliza shukrani zako za dhati na kueleza kwamba uko tayari kuitwa katika usaili. Unaweza kumaliza kwa kutaja nyaraka ulizoambatanisha pamoja na barua hiyo kama vile vivuli vya vyeti, wasifu binafsi na cheti cha kuzaliwa.
Mambo ya kuepuka
Unapoandika barua muhimu kama ya kazi, tumia maneno yanayojenga taswira ya mtu aliyetulia, mwenye heshima na uelewa, anayeweza kuuelezea uwezo wake vizuri bila kuonyesha majivuno yasiyo ya lazima. Epuka kutumia maneno ya amri, yasiyoonyesha unyenyekevu na maneno ya mtaani.
Pia, hakikisha lugha unayotumia ni fasaha, inaeleweka na haina makosa ya kiuandishi. Epuka makosa ya kisarufi kwani yanatoa picha ya mtu mzembe na mvivu, hivyo yanaweza kukugharimu hata kama ni kweli sifa za kitaaluma unazo.
Kumbuka, si sifa za kitaaluma pekee hutumika kufanya maamuzi ya kukuita kwenye usaili.
Aidha, huna haja ya kujitambulisha na kutoa taarifa zisizo za lazima na ambazo ulizitaja kwenye wasifu utakaouambatanisha.
Kwa mfano, haifai kujaza karatasi kwa maelezo kama: “Mimi ni kijana wa kiume mwenye miaka 24 nilizaliwa kwenye kijiji cha Kwa Mtoro wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma. Nimesoma shule ya Chekechea wilayani Rorya, na kisha nikahamia Kyela kwa masomo ya shule ya msingi mpaka darasa la pili kisha ...nikahamia shule ya msingi Lomwe, kisha nikaenda....”. Maelezo haya yanaonyesha huna ubunifu wala mbinu za kuwasiliana.
Mwisho na muhimu, ni makosa ya kujitakia kushawishika kutoa taarifa za uongo ili kujenga taswira chanya isiyokuwapo. Uongo una gharama.

Fahamu kuwa kuomba kazi si kupata kazi. Hata usipoitwa kwenye usaili bado lipo tumaini. Usikate tamaa. 
JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top