Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na fedha, ukiona mpenzi wako anaweka fedha mbele na ukishindwa kumpatia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.
Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze ukweli kisha muangalie namna nyingine ya kumsaidia.
Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe ‘out’, bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana fedha au laah.
Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba fedha kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo siyo ya msingi, tumia mbinu zifuatazo ni muhimu kuzifuata.
KWANZA; MWELEZE UKWELI
Kama huna fedha wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile.
Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana fedha au hana. Maana kuna wengine ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza ‘mizinga’.

PILI; JENGENI KUSAIDIANA
Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa. Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya basi analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake.
Inabidi Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna fedha zinavyokuwa hazitoshi na ataweza kubana matumizi.

TATU; ACHA UFUJAJI
Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa fedha kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa unazo!
Unachotakiwa ni kudhibiti mapema matumizi yako hata kama fedha itakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakushibishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri kumbe ni kapuku tu.

ZINGATIA HII
Mapenzi si kukomoana, bali kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku na wewe ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga mizinga mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.
JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top