1. Tuanzie hukoo Arusha
KAMA wewe unadhani huna fedha, basi kuna wengine ambao wamezichimbia Ardhini, tena kwa Mamilioni.
Benki ya chini ya ardhi iliyosheheni mamilioni ya fedha, zilizoswekwa ndani ya mifuko myeusi ya plastiki na kufukiwa mchangani, imechimbuliwa na matrekta ya kutengeneza barabara jijini Arusha huku noti nyekundu zikitawanywa kila kona na kufanyika kuwa 'Sadakalawe - Amina,' kwa kila mpita njia ambaye angeweza kujitwalia fungu.
Ilikuwa ni mshikemshike katika eneo la Mianzini Jiji Arusha, ambako kuna mradi mkubwa wa upanuzi wa barabara ya kutoka Mianzini Mataa hadi Ilkiding'a
Watu walipigana vikumbo katika harakati za kujineemesha na fedha zilizokuwa zimetapakaa eneo hilo. Ikiwa imesheheni noti tupu, tena nyekundu na mpya, kufumuliwa kwa akaunti hiyo ya benki ya chini ya ardhi pamoja na kuwa neema kwa wapita njia na wakazi wa eneo hilo, kuligeuka pia kuwa kilio kwa mmiliki wa hazina hiyo, Christopher Akoonay maarufu kama 'Mmbulu' ambaye sasa amejipatia jina jingine la 'Mabulungutu.'
Akonaay ni mkulima, lakini hasa akijishughulisha na ufugaji wa Ng'ombe wa Maziwa. Yeye hudamka asubuhi kukamua mifugo na kisha kusambaza bidhaa hiyo ya maziwa katika maeneo mengi ya jiji katika kuwauzia wakazi wa Arusha.
Na katika siku ya tukio, Akonaay alikuwa yuko kwenye shughuli zake za kuwapelekea maziwa wateja wake, ndipo watengeneza barabara walipofika eneo hilo la Mianzini na tingatinga zao na kuanza kuichimba njia hiyo ya kutoka Mianzini hadi Ilkiding'a katika kata ya Ilboru, inayotenganisha Jiji la Arusha na wilaya ya Arumeru.
Ikiwa imejengwa kwa fito na matope, nyumba ya 'Mmbulu' ilikuwa miongoni mwa zile zilizobomolewa na ni baada ya wamiliki wake, kugoma kuzibomoa wenyewe ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Akonaay amesema shauri lao walilipeleka Mahakamani kudai fidia kabla ya mradi wa Barabara haujapita hapo, Akonaay ameongeza kuwa mara baada ya kesi yao kutupiliwa mbali na chombo hicho cha Sheria, Wajenzi hawakusubiri hata saa moja ipite, bali walikwenda moja kwa moja eneo hilo na kuanza kazi.
Baadhi ya wakazi wa Mianzini, wamezungumzia suala hilo kwa masharti ya kutotajwa majina, wamesema ni ajabu kwa Mzee Akonaay kuwa na kiasi kikubwa cha fedha na kuzifukia ardhini huku mwenyewe akiishi kwenye nyumba duni ya matope.
Lakini Akonaay ambaye kwa sasa anaitwa 'Mabulungutu,' amesema kuwa alikosa Imani na Benki maana wakati akifanya kazi serikalini miaka ya 1980, alifungua akaunti na akawa anaweka fedha zake zote benki.
Baada ya kustaafu mwaka 1994 na kuamua kushughulika na ufugaji, hakuzifuatilia tena fedha zake benki hadi mwaka 2000, ambako alipokwenda kuangalia fedha zake aliambiwa kuwa kwa sababu akaunti yake haikuguswa kwa zaidi ya miaka 10, alitakiwa aende Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujieleza. Hata hivyo, aliona huo ni usumbufu na kuamua kuanza kuweka fedha zake Nyumbani.
Lakini hii pia ilimtokea puani baada ya mmoja wa ndugu zake kuzikwapua zote mara baada ya kuzifuma katika vitita vyenye thamani ya Sh milioni 20 na zaidi. Sasa Akonaay akaja na mkakati mpya wa kuhifadhi fedha kwa kuchimba shimo katikati ya chumba chake cha kulala, kilichokuwa upande wa barabara ya Mianzini na kuanza kuweka hazina yake humo.
Lakini tena, bahati mbaya ikiendelea kumuandama, Makatapila ya wachonga barabara, yakaifukua benki yake hiyo ya Ardhini na kutawanya fedha zaidi ya Sh milioni 35 zilizoishia kuokotwa na wapita njia pamoja na majirani, ambao kwa hofu hawakupenda hata kulizungumzia sakata hilo.
*…………………..*…………………….*………………………..*
2.
WALIMU wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere waliohusika kumpiga vibaya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mbeya wamefukuzwa chuo huku Jeshi la Polisi mkoani Mbeya likiwashikilia kwa mahojiano walimu wengine watano wa shule hiyo kutokana na tukio hilo.
Aidha, Serikali imemvua madaraka Mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kwa kutochukua hatua baada ya kitendo hicho kufanyika shuleni hapo Septemba 28, mwaka huu.
Hatua hizo zimechukuliwa baada ya Jumatano Octoba5 katika mitandao ya kijamii kusambaa kipande cha video kikionesha walimu zaidi ya watatu wakiwa eneo la ofisi wakimshambulia kwa kumpiga makofi, mateke na fimbo sehemu mbalimbali za mwili hasa kichwani mwanafunzi Sebastian Chinguku.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametangaza kuwafukuza chuo walimu wanafunzi hao walioshiriki kitendo cha kumpiga mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu wa Shule ya kutwa ya Sekondari ya Mbeya.
Walimu hao ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi huyo kwa makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa Duce na Evans Sanga wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Jumatano Profesa Ndalichako amesema kitendo hicho ni cha kikatili,  na kuwa walimu hao wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hiyo ya ualimu na kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Profesa Ndalichako amesema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu kitendo kilichofanywa na Walimu wanafunzi hao ni kosa la jinai na kuwa hakiwezi kufumbiwa macho.
Vilevile ametoa onyo kali kwa Wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na kwenda kinyume cha taaluma yao kuwa wanapoteza sifa hivyo amewataka kuzingatia maadili ya fani na taaluma wanazosomea.
Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Dhahiri Kidavashari amesema wanawashikilia walimu wa shule hiyo watano kwa mahojiano kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, amesema si kwamba walimu hao wanaohojiwa ndio waliohusika na tukio hilo bali wameanza na wale waliopo ili kupata taarifa zaidi.
Akieleza sababu ya Adhabu hiyo, Kamanda amesema katika mahojiano ya awali imebainika kuwa Mwalimu wa Kiingereza alitoa kazi, lakini baadhi ya wanafunzi hawakufanya baadaye mwalimu huyo aliwapa adhabu ya kupiga magoti, lakini mwanafunzi huyo alionekana kupinga kwa kueleza ana tatizo la goti hatoweza kufanya adhabu hiyo na mwalimu aliamua kumpeleka ofisini na kumpiga kwa kumchangia.
Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema Septemba 28 mwaka huu, mwanafunzi Chinguku wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Mbeya, Mkazi wa Uyole, alipigwa na walimu watatu.
Naye Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ameagiza mamlaka za nidhamu kumvua madaraka Mkuu wa Shule hiyo, Haule kwa kushindwa kuchukua hatua na kutoa taarifa mara baada ya tukio hilo kufanywa na Walimu Hao shuleni hapo.
George Simbachawene amevishauri vyuo vya Ualimu Viweke mkazo katika kufundisha Walimu vijana namna ya kuwa zaidi ya Walimu, kuwa na uvumilivu, subira na kuzingatia sheria. Wafunzwe kisaikolojia kukubali kuwa hawaishii kuwa walimu bali wanaingia kwenye kundi la malezi.
*…………………………*………………………….*……………………………*

3.
BAADHI ya Wachumi nchini wameitabiria neema Tanzania baada ya Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, kuihakikishia Tanzania kuwa mizigo yote ya DRC itapitia katika Bandari ya Dar es Salaam. Pamoja na hayo, wachumi hao wametahadharisha Serikali ya Awamu ya Tano, sasa kuanza kuwajibika ipasavyo kwa kutengeneza mazingira mazuri ya bandari hiyo, ikiwemo mifumo mbalimbali ya miundombinu ili kuweza kuvutia zaidi nchi nyingine kutumia Bandari za Tanzania.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja, amesema ziara ya Rais Kabila ni neema kwa Tanzania endapo tu serikali kupitia taasisi zake zitajipanga vyema kuboresha zaidi huduma za Bandari na maeneo mengine.
Amekiri kuwa nchi ya DRC imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania na mambo mengi. Lakini, katika suala la kibiashara ni vyema Tanzania ijipange, ingawa kijiografia nchi hiyo inaitegemea zaidi Tanzania kuliko Tanzania inavyoitegemea katika suala la Bandari.
Mtaalamu huyo amesema ziara hiyo imeibua mambo mazuri kwa nchi yetu, tukiyatumia vizuri uchumi wetu utapaa na sisi kuwa sehemu ya nchi zenye huduma bora za Bandari. Jambo la msingi lazima tuwajibike na kutambua kuwa maendeleo ya wenzetu yanatutegemea sisi
Amesema DRC haihitaji bandari pekee bali inahitaji huduma nyingine kama vile mfumo mzima wa miundombinu kama vile Barabara, Meli, Reli na Ziwa Tanganyika.
Vile vile Mtaalamu huyo amepongeza hatua ya Rais John Magufuli, kuanza kwa kutoa msamaha kwa mizigo ya DRC na kuiongezea muda kutoka siku 14 hadi 30 na kubainisha kuwa pamoja na kwamba itakuwa na hasara kidogo kwa serikali, lakini itawavutia zaidi wafanyabiashara wa nchi hiyo.
Kwa upande wake, Dk John Mtui ambaye naye ni Mtaalamu wa uchumi kutoka UDSM, amesema kupitia ushirikiano huo wa DRC na Tanzania, Watanzania watarajie mambo mengi mazuri ya kiuchumi. Hata hivyo, amesema ni wakati sasa kwa Serikali ya Tanzania kuanza kuharakisha ujenzi wa reli ya kisasa ya 'standard garage' itakayokuwa msingi na kiunganishi kikuu cha Biashara baina ya nchi hizo mbili.
Amesema anatambua kuwa Serikali ya Tanzania imekopa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Reli hiyo na kufafanua kuwa, deni la fedha hizo linaweza kurejeshwa na Uchumi kukua kwa kasi, endapo huduma za Bandari zitavutia kuliko Bandari nyingine.
Zile changamoto kama vile kuchelewesha mizigo, Rushwa iliyokithiri na Urasimu Bandarini na maeneo ya Usafirishaji zikidhibitiwa, Uchumi wa Tanzania unaweza kubadilika kuliko inavyotarajiwa.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa Malori mengi ya mizigo yanasafirisha mizigo hiyo kwenda na kutoka DRC, hivyo kukamilika kwa Reli hiyo, kutapunguza gharama kwa nchi hiyo na nyingine za jirani na hivyo kuvutiwa zaidi kuitumia bandari ya Tanzania.
Rais Magufuli ameahidi kuboresha zaidi Mazingira ya huduma ya Bandari hiyo na kusisitiza kuwa Idadi ya mizigo kutoka DRC imeongezeka na kufikia asilimia 10.6 ambapo hadi sasa Biashara baina ya nchi hizo imeongezeka kutoka Sh bilioni 23 mwaka 2009 hadi Sh bilioni 396.3.
*……………………….*…………………….*………………….*

4.
Na tuelekee huko Dar es salaam
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imejipanga kuzishughulikia na kuzimaliza changamoto zinazowakabili Wafanyabiashara ndogo nchi nzima ikiwemo Kariakoo ili kuwawezesha kufanya Biashara katika mazingira bora bila usumbufu.
Samia amesema hayo alipokuwa akizindua Jumuiya ya Wanawake Wajasiriamali na Biashara Kariakoo (JUWABIKA), jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali inajua kuwa Kariakoo ni kitovu cha Biashara, pia inatambua changamoto zinazowakabili Wafanyabiashara hao hususan zinazowagusa wanawake na akinamama ndio maana imejipanga kuzishughulikia.
Amesema pia inatambua ugumu uliokuwepo kwa Wafanyabiashara wadogo kupata mikopo ya kujiendeleza kutoka katika benki na taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo riba kubwa na masharti magumu ya ukopeshwaji.
Samia amesema kuhusu fursa za Mikopo, vilevile anaendelea kutoa wito kwa Benki kuona namna bora ya kuwakopesha Wafanyabiashara wadogo kwa masharti nafuu ili wakuze Mitaji yao, Serikali itahakikisha fursa ya mikopo kwa ajili ya mitaji inapatikana bila Urasimu na kwa masharti nafuu na kuwafikia Wananchi wengi mijini na vijijini.
Amewashauri pia wanawake kuwa mbele katika ulipaji wa kodi za Serikali kwani kodi hizo ndio zinazosaidia katika shughuli za maendeleo, kusomesha watoto na dawa hospitalini.
Awali Mke wa Rais wa Awamu ya Nne, Mama Salma Kikwete aliwataka wanawake hao wanaotokea eneo la Kariakoo wasisite kueleza changamoto zao pale wanapokumbana nazo kwa kuwa wanatoa pato kubwa kwa serikali kupitia kodi wanazolipa.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mwamvua Kinanda ameeleza changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni mtaji, ukosefu wa elimu ya Ujasiriamali na Biashara, uwepo wa machinga katika maeneo yao ya Biashara, Mlolongo wa kodi pamoja na Riba kubwa katika Benki.
*………………………..*…………………….*…………………*

5.

RAIS John Magufuli amewapongeza viongozi na wafuasi wa Madhehebu ya Bohora kwa kutumia maadhimisho ya Tamasha la Mabohora Duniani kuhimiza amani, upendo na mshikamano.
Aidha amewashukuru kwa kushiriki katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwemo mchango wa Dola za Marekani 53,000 zilizotolewa na Kiongozi Mkuu wa Bohora kwa Serikali kwa ajili ya kuchangia kampeni ya utengenezaji wa Madawati, na kuwaleta Madaktari kutoka Hospitali ya Saifee ya India waliotoa Matibabu bure kwa wananchi wa Arusha.
Ameyasema hayo wakati akihutubia katika Tamasha la Madhehebu ya Bohora ambayo yanafanya Maadhimisho ya dunia ya sikukuu ya mwaka mpya wa Kiislamu jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yaliwaleta nchini wafuasi zaidi ya 30,000 kutoka nchi mbalimbali duniani na kuongozwa na Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani, Mtukufu Dk Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb (TUS).
Amehutubia wafuasi wa Bohora katika Msikiti wa Hakimi uliopo Upanga jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amemshukuru Kiongozi Mkuu wa Bohora kwa kukubali kufanya maadhimisho ya mwaka mpya wa madhehebu hayo hapa nchini.
Amewashukuru pia na kuwapongeza Wafuasi wa Madhehebu hayo kwa kukubali kuja nchini na kukaa kwa siku zote za Maadhimisho yaani kuanzia Oktoba 2 walipoanza hadi Oktoba 11, watakapomaliza.
Aidha, Rais Magufuli amewakaribisha wafuasi wa Bohora duniani kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, Uvuvi, Misitu, Mifugo, Madini na Gesi kwani soko la uhakika lipo ndani ya nchi, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye watu takribani milioni 400.
Dk Saheb amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na wafuasi wa madhehebu ya Bohora katika maadhimisho hayo

6.
Na huko Afrika ya Kusini
Maandamano ya Amani ya Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Afrika Kusini yamegeuka kuwa fujo baada ya Jeshi la polisi kuingilia kati ili kuvuruga maandamano hayo mjini Johannesburg.
Shirika la Habari la IRNA limeripoti kuwa, mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu walifanya maandamano ya amani juzi Ijumaa kulalamikia siasa za Serikali ya Rais Jacob Zuma na Mazingira yao ya Masomo, lakini maandamano hayo yaligeuka kuwa fujo baada ya polisi kuingilia kati.
Wanafunzi hao wametaka kuongezewa posho zao huku Wanafunzi wenye asili ya Afrika Kusini wakiitaka serikali iwasomeshe bure.


Hii ni katika hali ambayo, gharama za masomo katika vyuo vikuu vya Afrika Kusini ni kubwa sana kiasi kwamba wenyeji wengi wa nchi hiyo hawawezi kuyamudu.
Kwa mujibu wa Habari hiyo, mazungumzo ya wakuu wa vyuo vikuu vya Afrika Kusini na Wawakilishi wa vyama vya wanachuo yameshindwa kuzaa matunda, na matakwa ya wanafunzi hao hayajakubaliwa.
Viongozi wa Afrika Kusini nao wametaka maandamano hayo yasitishwe mara moja ili wazuie kufungwa vyuo vikuu ambavyo wanafunzi wake wataendelea na migomo na maandamano.
*……………………………*……………………*……………………….*

7.
Wasichana wenye umri wa kati ya miaka 5 na 14 wanatumia asilimia 40 zaidi ya muda au saa milioni 160 kwa siku kufanya kazi za Nyumbani zisizo na malipo kote duniani.
Kazi hizo ni pamoja na kuteka maji na kusenya kuni, ikilinganishwa na Wavulana, Imesema ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyotolewa, kabla ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike itakayoadhimishwa Jumanne ya Oktoba 11.
Ripoti hiyo yenye lengo la Kuimarisha Uwezo wa Takwimu kwa ajili ya Wasichana na Kuorodhesha idadi na kuangalia mbele kwa ajili ya ajenda ya mwaka 2030, Inajumuisha makadirio ya kwanza ya dunia ya wakati unaotumiwa na Wasichana kufanya kazi za nyumbani kama vile kupika, kusafisha, kutunza familia, kuteka maji na kusenya kuni.
Ripoti inaonyesha kwamba, tofauti hiyo huanza mapema na mara nyingi kazi zinazofanywa na mtoto wa kike hazionekani na hazithaminiwi. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Somalia, Burkina Faso na Yemen, huku utafiti ukitaja kuwa wasichana weye umri wa miaka 10 na 14 Kusini mwa Asia, Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini hutumia muda mara mbili kufanya kazi za nyumbani kuliko wavulana.

Mwandishi wa ripoti hiyo Claudia Cappa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) amesema, Kutofautiana kwa  kazi hizi za nyumbani kunaonyesha kwamba jukumu la msingi la mtoto wa kike ni kuwa nyumbani na kufanya kazi hizo. Na hii inawafanya kutojitegemea kiuchumi
 Bi Claudia amependekeza kuwa, Ni muhimu kwamba sisi tunawekeza kwa wasichana katika uwezo wao na kuhakikisha kwamba wanakua kwa kujiamini na kujihisi kuwa na nguvu katika maisha yao. Na ni muhimu pia kuziimarisha jamii na familia ili kuzipa msaada muhimu wa kuwasaidia wasichana
*………………….*……………….*………….....*

8.
Mwakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ametahadharisha kuhusiana na vifo vya watoto nchini Uganda.
Aida Girma amesema hayo katika ripoti iliyopewa jina la "Hali ya Watoto Duniani Katika Mwaka 2016" na kusisitiza kwamba, katika hali ya hivi sasa watoto 127 hufariki dunia kila siku nchini Uganda kutokana na Maradhi mbalimbali kama Malaria.
Amesema kuna haja ya kufanyika juhudi maradufu na kwa kutumia suhula zilizopo nchini humo ili kuboresha hali ya mamia ya maelfu ya watoto wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mwakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF amesisitiza kuwa, shirika hilo linafanya juhudi kuhakikisha kwamba, Uganda iwe ni nchi ambayo watoto wake wanapata haki za awali na za kimsingi, kusiweko na watoto wanaokabiliwa na njaa nchini humo na mtoto yeyote asipoteze maisha kutokana na Maradhi ambayo yanaweza kutibika.
Takwimu zinaonesha kuwa, kuna takribani watoto milioni nane nchini Uganda ambao wanaishi katika umasikini na kwamba, kuna haja ya kuwekwa mikakati ya kuwaokoa watoto hao katika kipindi cha miaka 25 Ijayo.
Aidha kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni kabisa, Uganda ina Wakazi karibu Milioni 38 ambapo nusu yao wana umri wa chini ya miaka 15.
*………………*…………………*……………….*…………..*

9.
Na sasa tuelekee huko Sudan

Serikali ya Sudan Kusini imewataka wapiganaji wa Riek Machar, Makamu wa zamani wa rais na kiongozi wa waasi, kurejea Juba, mji mkuu wa nchi hiyo.
Naibu Waziri wa masuala ya Habari Nchini Sudan Kusini, Paul Akol Kordit ametoa wito huo hapo juzi akiwataka askari 750 watiifu kwa Riek Machar, kurejea mjini Juba kwa ajili ya kujiunga na Jeshi la Serikali. Akol Kordit ameongeza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari imechukua uamuzi wa kuwaondoa askari hao. Amesisitiza kuwa, Jumanne iliyopita Serikali ya Juba iliwataka askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo DR kushiriki kuwafukuza askari hao 750 kutoka katika nchi hiyo jirani.

Askari hao waliondoka Mjini Juba mwezi Julai mwaka huu baada ya kushamiri mapigano kati ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiira na Machar, mapigano ambayo yalisababisha mamia ya watu kuuawa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi.
Naibu Waziri wa masuala ya Habari nchini Sudan Kusini, Paul Akol Kordit amezitaka nchi za eneo  hilo kuiunga mkono Serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Riek Machar ambaye kwa sasa yuko Mjini Khartoum, Sudan amewataka wafuasi wake kuanzisha mapigano dhidi ya Serikali Ya Rais Salvar Kiir huku akisema kuwa, makubaliano yaliyofikiwa mwezi Agosti mwaka jana hayana tena itibari yoyote.
*………………………*……………………*………………………..*
10.
Maandamano ya wananchi Waislamu wa Nigeria wanaotaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria yameendelea kushuhudiwa nchini humo licha ya ukandamizaji wa vikosi vya usalama dhidi ya Waandamanaji.
Jimbo la Kaduna kwa mara nyingine tena limeshuhudia maandamano makubwa ya kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa korokoroni na vikosi vya usalama kwa karibu mwaka mmoja sasa.
Wananchi wa Kaduna juzi Ijumaa waliandamana na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Mwanazuoni huyo wa Kiislamu na kutoa wito wa kuachiliwa huru haraka mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Kama ilivyokuwa katika maandamano mengine ya kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Zakzaky, maandamano ya juzi pia mjini Kaduna yalishuhudia jeshi la Nigeria likiingilia kati na kuwatawanya waandamanaji hao kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za blastiki.

Ikumbukwe kuwa kati ya Disemba mwaka 2015, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Sheikh Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo.
*…………………..*…………………*…………………………*

11.
Watu zaidi ya 160 wameuawa katika mji mkuu wa Yemen Sana'a baada ya ndege za kijeshi za Saudi Arabia kuwashambulia raia waliokuwa katika shughuli ya mazishi.
Ripoti zinasema kuwa, watu wasiopungua 160 wameuawa katika mashambulio kadhaa yaliyofanywa na ndege za kijeshi za Saudia dhidi ya waombolezaji waliokuwa katika shughuli ya mazishi mjini Sana'a, jana Jumamosi alasiri.
Shirika la Habari la Xinhua limeripoti kuwa, watu 160 wameuawa kwa umati katika shambulio hilo la ndege za kijeshi za Saudia. Ripoti zaidi zinasema kuwa, miongoni mwa waliouawa wapo maafisa wa ngazi za juu wa Yemen.
Aidha mamia ya watu wameripotiwa kujeruhiwa katika jinai hiyo huku kukiweko na uwezekano wa idadi ya vifo kuongezeka. Baadhi ya duru zimeyataja mashambulio ya leo ya ndege za Saudia dhidi ya waombolezaji waliokuwa katika shughuli ya mazishi kwamba, ni mauaji ya umati.
Septemba mwaka jana pia, ndege za kijeshi za Saudia zilishambulia sherehe ya harusi na kuua kwa umati watu wasiopungua 130. Mashambulio na jinai za Saudia na washirika wake zinaendelea kila uchao dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen huku Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama zikiwa zinanyamazia kimya ukatili huo.

Tangu Ilipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka uliopita, hadi sasa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud na kuungwa mkono na Marekani na Israel umeshazishambulia skuli, hospitali, makaazi ya raia misikiti, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo. Zaidi ya watu 10,000 wamepoteza maisha katika hujuma ya kinyama ya Saudia dhidi ya Yemen
 
Top