muonekano wa daraja la mungu |
WILAYA ya Rungwe Jijini Mbeya ina
mambo mengi ya kustaajabisha na miongoni mwa mambo hayo yapo kwenye Mto Kiwira
.
.
Mto Kiwira unazidi kupanda
chati kuliko mito mingine wilayani humo kutokana na kuwapo kwa Daraja la Mungu.
Lakini pia karibu na daraja
hilo yapo maajabu mengine yakiwamo ya chekeche la uchafu unaokusanywa na
maji kabla ya kuingia eneo maarufu la Kijungu.
Kijungu nayo ni sehemu ya Mto
Kiwira, ni eneo la ajabu kwa sababu mwamba wake umeumba kitu kama chungu
kinachopokea maji yote na kuyapeleka chini bila kupitisha juu ya mwamba.
Inaelezwa kwamba mtu anayetaka
kuvuka salama kwenye mwamba juu ya Kijungu kutoka upande wa Mashariki lazima
atumie mguu mmoja wa kulia na akitokea Magharibi atumie mguu wa kushoto tu ili
asitumbukie.
Maajabu mengine ni kuwapo kwa
taarifa zinazodai mtu akizama kwenye mto huo, lazima afuatwe mzamiaji mmoja
aliyerithi kazi hiyo kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa kimila na kwamba bila
huyo, aliyezama hawezi kuonekana mpaka siku saba zitakapopita.
Lakini jambo kubwa linaloonekana na
kustaajabisha ni kuwapo kwa daraja linaloaminiwa na wakazi wa eneo
hilo na wilaya nzima ya Rungwe kwamba lilitengenezwa na Mungu kwenye eneo
la Mto Kiwira unapotenganisha Vijiji vya Lugombo kwa upande wa Mashariki
mwa mto huo na kile cha Mboyo kilichopo Magharibi.
Mto Kiwira ni mojawapo ya mito minne
inayotoka Mlima Rungwe kupeleka maji kwenye Ziwa Nyasa.
Mito mingine inayopeleka maji kwenye
Ziwa Nyasa ni Lufilyo, Mbaka na Songwe, lakini kila mto una sifa za
maajabu yanayotofautiana
Mto Kiwira unatofautiana na mito
mingine kwa mambo mengi yakiwamo ya kuwa mto wenye urefu wa karibu kilometa 70
kutoka chanzo chake kilichopo Mlima Rungwe hadi Ziwa Nyasa na pia upo chini ya
ardhi kwa umbali wa karibu kilometa mbili kutoka usawa wa Mji wa Tukuyu
ambao ni makao makuu ya wilaya hiyo.
Mto Kiwira umepewa jina hilo
kutokana na matawi mengi ya mto huo kupitia karibu na Mji Mdogo wa Kiwira ambao
ni maarufu kwa kuuza matunda mbalimbali kwa bei poa wilayani Rungwe.
Sehemu kubwa ya maji ya mto
huo yanaonekana kuwa meupe kutokana na kuwapo kwa maporomoko madogo madogo
mengi yanayopitisha maji kwa kasi inayokadiriwa kuwa kilometa 50 kwa saa.
Lakini pia yapo mabwawa ya mto huo
yaliyotuama kiasi cha watu wegi kujiuliza kama maji yamesimama ama yanaendelea
mbele.
Kwa upande mwingine, mto huo pia
unafanya kazi moja ya kiserikali ya kugawa mpaka wa vijiji katika Wilaya ya
Rungwe, na pia unagawa mpaka wa Wilaya za Rungwe na Ileje , Kyela na Ileje
kabla ya kuingia Ziwa Nyasa.
Umbile la Daraja la Mungu
Kama nlivyokueleza hapo awali, Mto
Kiwira upo chini zaidi ya ardhi ya Wilaya ya Rungwe na una maajabu mengi,
lakini moja wapo ni la kuwapo kwa daraja linaloaminiwa kuwa la Mungu
linaunganisha vijiji vya Lugombo na Mboyo Kata ya Lufingo , wilayani
Rungwe.
Daraja hilo limeundwa kwa mwamba wa
mawe ukiwa na urefu wa karibu mita 12 na upana wa wastani wa mita tatu.
Kwa mujibu wa kijana Christopher
Suleiman ambaye ni mwongozaji wa watalii wanaofika wilayani humo kupitia
kampuni ya Rungwe Tea and Tours , watalii wengi wanafika na kukiri kwamba
daraja hilo ni kubwa zaidi kuliko madaraja mengine ya asili yaliyopo duniani.
Suleiman anasema Daraja la Mungu
linatembelewa na wazungu wengi kutoka nje kupitia kampuni anayofanyia
kazi lakini pia wapo wanafika wenyewe.
Ukitaka kwenda darajani hapo,
ukitokea jijini Mbeya utapita barabara kuu ya Mbeya kwenda Kyela na
utateremkia Kijiji cha Kyimo maarufu kwa jina la ‘KK’ ambapo utapata
usafiri wa pikipiki au magari ya kukodi kukupeleka kwenye shimo la Mto
Kiwira umbali wa kilometa karibu 10 kutoka barabara kuu
Katika safari ya kwenda huko utaiona
Sekondari ya Iponjola na baada ya hapo utaingia Kijiji cha Lugombo na
kuikuta Sekondari ya mchepuo wa Kiingereza ya God’s Bridge International School
ambayo imeanzishwa miaka mitatu iliyopita ikiwa na jina hilo ili kuenzi
Daraja la Mungu.
Safari itaendelea Ukianza
kuukaribia mto, utaona kwa ng’ambo majengo mengi mazuri yaliyotuama
umbali wa kilometa moja chini ya miti pembezoni mwa Mto
Kiwira.
Majengo hayo ni ya Chuo cha Askari
Magereza Tanzania .Kwa asilimia kubwa majengo ya chuo hicho yapo
pembezoni ya Mto Kiwira , lakini kabla ya kuuvuka mto kupitia daraja
lillilojengwa na Serikali utapinda kushoto kuekelea kwenye Daraja la
Mungu.
Baada ya mita 400 hivi
utalikuta daraja lingine ambalo linaelezwa kwamba lilijengwa na Warusi
waliopewa kazi ya kujenga mtambo wa kufua umeme kwenye maji yaendayo kasi
karibu na Daraja la Mungu.
Ukiwa kwenye daraja hilo
utaliona Daraja la Mungu likiwa kusini mwa mto ambalo limeundwa kwa umaridadi
wa aina yake.
Daraja hilo kwa chini
limejikunja kama upinde, lakini juu kukiwa na nafasi yenye upana
unaotofautiana, kwani lipo eneo lenye upana wa mita tano na mita mbili. Kwa
kweli ni la ajabu kwani hata maji yanavyokatisha eneo hilo yanatisha.
Kutisha kwake kunatokana na
maji hayo, badala ya kunyoka kulikatisha daraja, yanaelekea kwanza kwenye
mwamba uliopo mashariki na kuzunguka kuelekea kaskazini na hatimaye kuelekea
kusini yakiwa na kasi ndogo chini ya daraja hilo kabla ya kupokewa tena na
poroko lenye kasi linalotoa mvuke wakati wote.
Penye poromoko la maji hayo
panaelezwa kwamba Serikali iliwatafuta Warusi ili wasaidie kuweka mitambo ya
kufua umeme mwaka 1969 hafi 1978 walipofukuzwa kwa saa 24 bila kufanikisha
suala hilo
Uvumbuzi wa Daraja Mungu
Ni wazi daraja hilo ni la asili
kutokana na miamba ya Mwenyezi Mungu kuunganishwa na kuruhusu maji kupita chini
yake. Lakini ni nani aliyegundua daraja hilo?
Swali hili ni vigumu kujibiwa,
lakini kutokana na historia iliyotolewa na watu waliotangulia eneo hilo ni
kwamba wagunduzi wa kwanza walikuwa nyani.
Lusajo Mbwiga (30) ni mjukuu wa
aliyekuwa kiongozi wa mila wa eneo hilo aliyekuwa akiitwa Mwahesya.
Kijana huyo ndiye aliyechiwa mikoba
yote ya uchifu na hatimaye wanakijiji wa Mboyo kumridhia
kwa ujasiri wake katika kutambua mazingara na vituko vya Mto Kiwira.
Mbwiga ambaye kwa sasa anajulikana
zaidi kwa jina la Chifu, anaamini kwamba Mto Kiwira unaongoza kwa kuua
watu na anasema ndiye aliyebeba mikoba ya kuzama kwenye mto huo kuopoa maiti
yoyote inayopotea
Anasema kwa maelezo ya babu yake ni
kwamba Daraja la Mungu liligunduliwa na nyani.
‘’Baada ya nyani kupita waliofuata
nyayo za nyani walikuwa watu wa kabila la Waandali kutoka Wilaya ya Ileje
ambao awali walikuwa wakivuka mto huo kwa kuruka eneo lililoaminika kuwa na
maajabu na kuua watu wengi.
Eneo hilo linatajwa kuua
Waandali wengi kwa kutumbukia , lakini wachache walifanikiwa kuruka.
“Wachache walioruka waliamini kwamba
waliotumbukia hawakuruka kwa ujanja’’ alisema na kuongeza kwamba ndio maana
hapa panaitwa ‘’atanyerite bukomu’ ikiwa na maana kwamba hakuruka vizuri
ndio maana ametumbukia kwenye mto.
Kwa mujibu wa Mbwiga Waandali hao
walikuwa wakitoka Ileje huko Magharibi ya mto wakielekea Rungwe Mashariki
na walipofika hapo kiongozi wao aliruka akiwa na mnyama mbuzi aliyemfunga
mgongoni, lakini waliofuata walipojaribu kuruka walianza kutumbukia na kufa.
Eneo hilo ambalo pia ni la maajabu
ya Mto Kiwira lipo mita 800 kaskazini mwa Daraja la Mungu ambapo pia
limejengwa daraja ambalo sasa linatumika kwa watu na vyombo vya usafiri
kuunganisha Wilaya za Rungwe na Ileje.
Naye Mzee Brown Mwapulo (76)
ambaye ni kiongozi wa kimila Kitongoji cha Ibaga kwenye Kijiji ch Lugombo
anasema miaka ya 1930 hadi 1950 Waandali wengi walitumbukia eneo hilo na baada
ya kuona hivyo walianza kutafuta eneo lingine la kuvuka na hatimaye waliwaona
nyani wakivuka eneo la Daraja la Mungu na kuamua kuwafuata.
"Baada ya watu hao
kuliona daraja hilo, ikawa mwanzo wa kutumika na limekuwa likitumia hadi
walipokuja Warusi na kujenga daraja lingine karibu na eneo hilo’’ anasema.
picha ya kijungu kilichopo katika daraja la mungu |
Hali ya Daraja la Mungu kwa sas
Mwangalizi wa daraja
hilo, Mbwiga anasema Daraja la Mungu limeanza kupata misukosuko kutokana na mto
kuendelea kuchimba zaidi mwamba ambao kwa sasa unabomoka upande wa magharibi.
Pia anasema miti mikubwa
imeota juu ya daraja na kusababisha mizizi inayopasua mawe na hatimaye
yanayodondoka.
“Kwa ujumla “matunzo ya
kivutio hiki bado hayajapewa kipaumbele’’ anasema.
Hata hivyo anadokeza kwamba uongozi
wa Wilaya ya Rungwe umeshatamka kuboresha eneo la Daraja la Mungu na kwamba
tayari umetoa kitabu cha risiti ili kuwatoza watalii wanaotembelea eneo hilo.
“Wanafunzi wanaotembelea ni bure,
lakini watalii kutoka nje ya nchi wanatakiwa kulipa walau Dola 2 za Marekani
ambazo ni sawa na Sh 5,000
Kauli ya Kijiji ch Lugombo
Ofisa Mtendaji Wa Kijiji cha
Lugombo, Jana Bukuku anasema Daraja la Mungu limeisaidia ofisi hiyo kupata viti
vya ofisi kutokana na fedha zilizotolewa na Kampuni ya Rungwe Tea and Tours
baada ya kuwaonyesha daraja hilo.
Bukuku anasema mkakati ni
kushirikisha wananchi katika kutunza eneo hilo la utalii.
”Kutokana na watalii kuonekana
eneo la kijiji chetu , kwa sasa tuna mpango wa kuanzisha kituo maalumu cha
kuonyesha vitu mbalimbali vya kimila, mfano vilago,mavazi ya machifu , mikuki
ya zamani, nyengo , tezo, nguo za asili enzi za ukoloni maarufu kama
‘amaabi”,anasema.
Mkakati wa Serikali ya
Wilaya Rungwe
Mkuu wa wilaya hiyo, Chrispine
Meela anasema Daraja la Mungu ni moja ya vitutio vingi vya utalii
wilayani humo.
Meela anasema Serikali imeamua
kuyaweka wazi maeneo yote ya utalii yakiwamo ya Mto Kiwira naq maajabu yake.
“Januari 18, mwaka huu,
tuliunda kamati ya wadau 15 wa sekta ya utalii ambayo itaandaa uzinduzi maalumu
wa kutangaza vivutio vya utalii wilayani humo’’anasema.
Meela anasema kamati hiyo
imeshirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wenye hoteli, kampuni za kusafirisha
watalii, na wananchi baada ya kugundua wilaya ikiwa na vivuti vingi vizuri vya
utalii.
Anataja baadhi ya vivutio kuwa
ni Daraja la Mungu, Ziwa Ngozi, Ziwa Kisiba, Boma la Wajerumani Masoko,
Maporomoko ya Kaporogwe, Maporomoko ya Mto Suma kwenye Kijiji cha Malamba na
Mlima Rungwe ambao ni wa tatu kwa urefu baada ya Kilimanjaro na Meru nchini.