Kwanza tujue hivi Zaidi ya watu
milioni 120 ulimwenguni wana matatizo ya kusikia.kutokana na Shirika la Afya Ulimwenguni.
UWEZO wetu wa kusikia ni zawadi
inayopaswa kuthaminiwa. Hata hivyo, kadiri tunavyoendelea kuzeeka,
ndivyo uwezo
wetu wa kusikia unavyoendelea kupungua. Ulimwengu wa sasa unatokeza sauti
nyingi tofauti-tofauti na makelele ambayo yanaelekea kuharibu uwezo wa kusikia
mapema zaidi. Mwanasayansi mashuhuri katika Taasisi Kuu ya Viziwi huko
St. Louis, Missouri, Marekani, anasema kwamba Karibu robo tatu ya matatizo
ya kusikia ambayo Mwamerika mmoja anakabili yanatokana na yale ambayo
amesikiliza maishani mwake bali si kwa sababu ya uzee tu.
Kusikiliza sauti kubwa, hata kwa
muda mfupi kwaweza kuharibu sehemu za ndani za sikio lako zilizo nyororo. Hata
hivyo, mara nyingi, matatizo ya kusikia husababishwa na “kazi zenye makelele,
makelele unayosikia wakati unapofanya mambo unayoyapenda, na burudani zenye
kelele,”. Unaweza kufanya nini ili kulinda uwezo wako wa kusikia? Ili kujibu
swali hilo, ni muhimu kujua mambo fulani kuhusu jinsi uwezo wako wa kusikia
unavyofanya kazi.
Sauti
Tunazosikia
Mazingira tunamoishi yanazidi
kuwa na makelele mengi zaidi. Kila siku wengi wanakabiliana na sauti za aina
tofauti kuanzia za magari, mabasi, na malori barabarani, hadi sauti za juu sana
za mashine za umeme kazini.
Nyakati nyingine sisi huzidisha
tatizo kwa kuweka sauti za juu katika vifaa tunavyosikiliza. Njia moja ya
kusikiliza muziki inayopendwa na wengi ni kutumia vidude vya kusikiliza
vinavyovaliwa masikioni ambavyo vimeunganishwa na kifaa kinachobebeka cha kuchezea
kaseti au CD. Kulingana na Marshall Chasin, mmoja wa waanzilishi wa Vyama
vya Wanamuziki vya Kanada, uchunguzi uliofanywa nchini humo na katika Marekani
unaonyesha kwamba vijana wanaendelea kupoteza uwezo wao wa kusikia kwa sababu
ya kutumia vidude vya kusikiliza
muziki vinavyovaliwa masikioni huku wakiweka sauti ya juu kupita kiasi.
Ni
kiasi gani cha sauti kinachoweza kusemwa kuwa cha kupita kiasi?
Sauti inaweza kukadiriwa kwa kutumia vipimo
vitatu—muda wa kuisikiliza, frikwensi, na kiasi cha sauti yenyewe.
Muda wa kusikiliza ni kipindi cha wakati ambao
mtu anakabiliana na sauti fulani.Frikwensi
hupimwa kulingana na mizunguko ya sauti katika kila sekunde, au hezi.Vipimo vya
frikwensi ya sauti ya kawaida inayosikika vizuri ni kuanzia mizunguko 20
hadi 20,000 kwa kila sekunde.
Kiasi cha sauti, au ukubwa wake, hupimwa kwa kipimo kinachoitwa
desibeli (dB). Kiasi cha sauti cha maongezi ya kawaida ni dB 60 hivi.
Wataalamu wa sauti wanasema kwamba kadiri unavyosikiliza sauti inayozidi
desibeli 85, ndivyo unavyokabili uwezekano mkubwa zaidi wa kupoteza uwezo
wako wa kusikia. Kadiri sauti inavyozidi kuwa kubwa ndivyo inavyoharibu uwezo
wa kusikia haraka zaidi.
Ripoti moja katika gazeti la Newsweek inasema
hivi: “Sikio lako linaweza kustahimili kwa saa mbili iwapo unafanya kazi na
mashine ya umeme ya kutoboa mashimo (100dB), lakini haliwezi kustahimili zaidi
ya nusu saa katika chumba cha kuchezea michezo ya video chenye makelele mengi
(110dB). Kila ongezeko la dB 10 katika kiasi cha sauti linamaanisha kwamba
kelele inayoweza kuharibu sikio imeongezeka mara 10.” Utafiti
umethibitisha kwamba sauti za kuanzia dB 120 hivi husababisha uchungu. Jambo la
kushangaza ni kwamba redio fulani za nyumbani zinaweza kutoa sauti ya zaidi ya
desibeli 140!—Ona sanduku.
Ili kukusaidia kuelewa kwa nini
sauti kubwa zinaweza kuharibu uwezo wako wa kusikia, hebu tuchunguze kile
kinachofanyika sauti inapoingia masikioni mwako.
Jinsi
Masikio Yetu Yanavyofanya Kazi
Sehemu ya nje ya sikio ina umbo
ambalo huiwezesha kuchota mawimbi ya sauti na kuyaingiza kwenye mfereji wa
sikio, ambapo yanaweza kufikia kiwambo cha sikio. Mawimbi hayo hufanyiza
mitetemo katika kiwambo cha sikio, nacho hutokeza mitetemo kwenye mifupa mitatu
iliyomo katika sikio la kati. Kisha, mitetemo hiyo hupitishwa hadi kwenye sikio
la ndani, ambamo kuna kifuko kilichojaa umajimaji ambacho kinazingirwa na
mfupa. Katika sehemu hiyo mitetemo husafiri kupitia umajimaji ulio katika komboli, ambayo ni sehemu ya sikio la
ndani yenye umbo la konokono na ina chembe zilizo kama nywele. Umajimaji ulio
katika komboli huchochea sehemu ya
juu ya chembe hizo zilizo kama nywele ili zitokeze misukumo ya neva inayoweza
kutambuliwa.
Hatimaye misukumo hiyo ya neva husafirishwa
hadi kwenye ubongo ambamo zinageuzwa na kutambuliwa kuwa sauti.
Mfumo wa ubongo unaoshughulikia hisia na msukumo husaidia ubongo
kuamua ni sauti zipi zinahitaji kupewa uangalifu na ni zipi ambazo zitapuuzwa. Kwa kielelezo, huenda mama
asishughulike anaposikia sauti ya mtoto akicheza, lakini ataitikia mara moja
mtoto anapolia akiomba msaada. Kusikiliza kwa masikio yote mawili ni muhimu
sana kwani huturuhusu kupata sauti kwa njia nzuri kutoka pande zote na
hutusaidia kutambua upande ambao sauti inatoka. Hata hivyo, wakati wa
mazungumzo, ubongo wetu unaweza kuelewa ujumbe mmoja tu kwa wakati mmoja. Hiyo
ndiyo sababu, mtu anapoongea kwa simu, hawezi kusikia yale ambayo mtu mwingine
aliye karibu naye anasema.
Jinsi
Makelele Yanavyoharibu Uwezo Wetu wa Kusikia
Ili uelewe jinsi sauti kubwa
zinavyoharibu uwezo wetu wa kusikia, fikiria mfano unaofuata. Ripoti moja
kuhusu usalama kazini inafananisha chembe zilizo kama nywele katika sikio la
ndani na zao la ngano shambani na kulinganisha sauti zinazoingia humo na upepo.
Upepo mwanana, kama sauti ndogo, utafanya sehemu ya juu ya mmea wa ngano
kuyumbayumba, lakini ngano haitaharibika. Hata hivyo, upepo mkali utaongeza
mkazo kwenye shina la mmea wa ngano. Upepo mkali wa ghafula, au upepo mwanana
unaoendelea kwa muda mrefu waweza kuharibu mmea na kuufanya unyauke.
Tunaweza kulinganisha jambo hilo
na yale makelele yanayogonga chembe nyororo zilizo kama nywele katika sikio la
ndani. Mlio mkubwa wa ghafula unaweza kuharibu sehemu za sikio la ndani na
kuacha makovu ambayo huharibu kabisa uwezo wa kusikia. Zaidi ya hilo, sauti
kubwa zinazoendelea kwa muda mrefu zinaweza kuharibu kabisa zile chembe
dhaifu zilizo kama nywele. Zikiharibika, haziwezi kukua tena. Tokeo ni mvumo
sikioni—milio kama ya nyuki, kengele, au mngurumo unaosikika masikioni au
kichwani.
Sasa basi..
Linda
na Kudumisha Uwezo Wako wa Kusikia
Ingawa mtu anaweza kuzaliwa na
matatizo ya kusikia ama akayapata kupitia msiba usiotazamiwa, tunaweza
kujitahidi kulinda na kudumisha uwezo wetu wa kusikia wenye thamani. Ni jambo
la hekima kujifunza kuhusu hatari zinazohusika. Kama vile mtaalamu mmoja wa
sauti alivyosema, ‘kungojea mpaka tatizo litokee ndipo uchukue hatua ni kama
kuanza kutumia kifaa cha kuzuia mbu baada ya kuambukizwa malaria.’
Jambo la maana mara nyingi ni jinsi tunavyosikiliza
bali si kilatunachosikiliza. Kwa mfano, ukitumia vidude vya kusikiliza muziki
vinavyovaliwa masikioni, unaweza kuweka sauti ndogo ambayo inaweza kukuruhusu
kusikia sauti nyingine. Iwapo redio katika gari lako au nyumbani mwako
imefunguliwa sauti ya juu hivi kwamba huwezi kusikia watu wanapozungumza, hiyo
ni ishara ya kwamba sauti hiyo imepita kiasi na inaweza kuharibu uwezo wako wa
kusikia. Wataalamu huonya kwamba kusikiliza sauti ya desibeli 90 kwa muda
wa saa mbili au tatu kunaweza kuharibu masikio yako. Wanapendekeza kuvalia
vifaa vya kulinda masikio katika mazingira yenye makelele.
Wazazi kukumbuka kwamba ni rahisi
kwa watoto kuharibika masikio kuliko watu wazima. Kumbuka kwamba vitu vya
kuchezea vinavyotoa sauti za juu vyaweza kusababisha hatari. Kwani, vitu kama
hivyo vinaweza kutoa sauti ya desibeli 110 vinapotikiswa!
Masikio
yetu yana viungo vyororo, vidogo, na vya ajabu. Masikio hutuwezesha kusikia
sauti zote mbalimbali na zenye kupendeza katika mazingira yetu. Kwa kweli,
uwezo huo wa kusikia ambao ni muhimu sana unastahili kulindwa.