Ripoti mpya ya shirika la Save the
Children inasema msichana wa chini ya miaka 15 huozwa kila baada ya sekunde
saba duniani.
Ripoti hiyo inasema watoto wa hadi chini ya miaka 10
wanashurutishwa kuolewa na
wanaume wazee katika nchi kama vile Afghanistan,
Yemen, India na Somalia.
Save the Children wanasema ndoa za mapema zinaweza kuchangia
msururu wa matatizo ambayo huathiri maisha yote ya msichana.
Mizozo, umaskini na migogoro ya kibinadamu vinatazamwa kama
sababu kuu zinazowaweka wasichana hatarini ya kuozwa wakiwa bado wana umri
mdogo.
“Ndoa za mapema huanzisha msururu wa matatizo ambayo humnyima
msichana haki za kimsingi za kujifunza, kujikuza na kujivunia maisha yake kama
mtoto," amesema afisa mkuu mtendaji wa Save the Children International
Helle Thorning-Schmidt.
Wasichana wanaoolewa wakiwa wadogo mara nyingi huwa hawawezi
kuendelea na masomo, mara nyingi hudhulumiwa na waume zao, kupigwa na hata
kunyanyaswa kingono. Hupachikwa mimba na pia huwa hatarini ya kuambukizwa
magonjwa ya zinaa, ukiwemo Ukimwi.
Ripoti hiyo iliyopewa jina Every Last Girl, imeorodhesha nchi
ambazo ni ngumu zaidi kwa wasichana baada ya kuzingatia elimu, ndoa za watoto,
mimba za mapema, vifo vya wanawake wakijifungua na idadi ya wanawake bungeni.
Chad, Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na Somalia
zinashika mkia kwenye orodha hiyo.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto, Unicef,
linakadiria kwamba idadi ya watoto watakaoozwa wakiwa wadogo itaongezeka kutoka
milioni 700 kwa sasa hadi 950 milioni kufikia 2030.
Ripoti hiyo ya Save the Children imetolewa siku ya maadhimisho
ya Siku ya Msichana Duniani.