Wapinzani
nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekusanyika katika mji wa Kisangani
nchini humo wakitaka kuachiwa huru wanaharakati wa kisiasa wanaoipinga
serikali. Benjamin Ntumba mmoja
Benjamin Ntumba
mwanaharakati wa chama cha upinzani Kongo cha (UDPS)
Wanaharakati hao sita
wa kisiasa wanaoipinga serikali ya Kinshasa wanashikiliwa mahabusu huko
Kisangani tangu tarehe 19 mwezi uliopita hadi sasa. Benjamin Ntumba
ameashiria kuachiwa huru watu wengine ambao walitiwa mbaroni pamoja na
wanaharakati hao sita na kusisitiza kuwa, wanaharakati hao wa kisiasa
wanaoipinga serikali ya Kongo wamekatwa kinyume cha sheria. Ntumba ametaka
wanaharakati hao waachiwe huru haraka na bila ya masharti yoyote.
Na tukielekea huko Africa kusini ni kwamba..
Maandamano
ya wanachuo nchini Afrika Kusini yanaripotiwa kuongezeka baada ya baadhi ya
vyuo kufunguliwa.
Mamia ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Wits cha mjini Johannesburg
leo wameandamana wakilalamikia sera za serikali katika kushughulia hali ya
wanachuo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, barabara za Chuo Kikuu cha Wits leo
zimeshuhudia maandamano makubwa ambayo yameingiliwa kati na polisi na kupelekea
kutokea vurugu kubwa.
Vitendo vya vyombo vya usalama vya Afrika Kusini vya kutumia
mabavu dhidi ya maandamano ya amani ya wanachuo hao vinakithiri katika hali
ambayo, masomo katika vituo vingi vya elimu na Vyuo Vikuu yamesimamishwa
katika mji wa Johannesburg.
Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Afrika Kusini wamekuwa wakifanya
maandamano ya amani kwa muda sasa kulalamikia siasa za serikali ya Rais Jacob
Zuma na mazingira yao ya masomo.
Kilio kikubwa cha
wanachuo hao ni ongezeko kubwa la karo na takwa lao la kuongezewa posho.
Hata hivyo maandamano hayo ya amani ya wanachuo yamekuwa
yakizusha vurugo na fujo kati yao na vyombo vya usalama ambavyo vimekuwa
vikitumia mabomu ya machozi na risasi za blastiki kuwatawanya wanachuo hao.
Mara kadhaa kumefanyika mazungumzo ya wakuu wa vyuo vikuu
vya Afrika Kusini na wawakilishi wa vyama vya wanachuo lakini mazungumzo hayo
yameshindwa kuzaa matunda.
Na huko Israel
Afisa
wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema
kuwa, harakati hiyo itatoa jibu kali kwa shambulio lolote tarajiwa kutoka kwa
utawala haramu wa Israel.
Dakta Mahmoud al-Zahar ametangaza kuwa, Harakati ya Mapambano ya
Kiislamu ya Palestina HAMAS itajibu kwa nguvu zake zote jinai yoyote ile
itakayofanywa na utawala ghasibu wa Isarael dhidi ya wananchi wa Palestina.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Chama cha Hamas ameashiria
vitisho vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kusema kuwa,
endapo utawala huo ghasibu unataka kuanzisha vita vipya katika eneo, basi
mapambano na muqawama wa wananchi wa Palestina umejiandaa kukabiliana vilivyo
na uchokozi huo.
Amesema, mahesabu
ya Avigdor Lieberman, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel ya kutaka
kuishambulia Gaza ni propaganda zenye lengo la kutoa pigo kwa eneo hilo na
kuongeza kuwa, waziri huyo wa Kizayuni anataka kuzionesha fikra za waliowengi
katika jamii ya Wazayuni kwamba, utawala huo umetoa pigo kwa muqawama na
mapambano ya wananchi wa Palestina.
Mahmoud al-Zahar ameeleza kuwa, machafuko na vita vyovyote vile
katika mipaka ya Gaza na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu vitapelekea
maelfu ya walowezi wa Kizayuni kukimbia na ni kwa msingi huo, viongozi wa
Israel hawawezi kuanzisha vita vingine.
Tumalizie na huko niger
Ofisi
ya Rais wa Niger imetangaza siku mbili za maombolezo nchini humo baada ya
mauaji ya wanajeshi kadhaa katika shambulizi lililofanywa dhidi ya kambi ya
wakimbizi wa Mali huko kaskazini mwa Niger.
Taarifa iliyotolewa na
Ofisi ya Rais wa Niger imesema kuwa, nchi nzima itakuwa katika maombolezo ya
taifa kwa muda wa siku mbili baada ya mauaji ya wanajeshi 22 katika
shambulizi lililofanywa na kundi moja la watu waliokuwa na silaha dhidi ya
kambi ya wakimbizi wa Mali katika eneo la Tazalit.
Wizara ya Ulinzi ya
Niger imetangaza kuwa, askari 14 wa Gadi ya Rais, polisi 5 na wanajeshi 3 wa
nchi hiyo wameuawa katika shambulizi hilo na wengine watatu wamejeruhiwa.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Niger, Moustapha Ledru amesema kuwa, kundi
lililofanya mauaji hayo limekimbilia katika ardhi ya nchi jirani ya Mali
na kwamba, operesheni ya kuwasaka inaendelea. Maafisa usalama wa Niger
wanasema, shambulizi hilo limefanywa na kundi la kati ya watu 30 hadi 40 ambao
walikuwa wakizungumza lugha ya watu wa kabila la Tuareg.
Wakati huo huo
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Bi Nkosazana Dlamini Zuma amelaani
shambulizi hilo na kutoa salamu za rambirambi kwa serikali ya Niger na familia
za wanajeshi hao. Dlamini Zuma ametangaza tena upinzani wa Umoja wa Afrika
dhidi ya ukatili, ugaidi na misimamo mikali na kusema: AU itaendeleza jitihada
za kushirikiana zaidi na serikali ya Niger, nchi za eneo la Ziwa Chad na
jumuiya za kimataifa kwa ajili ya kupambana na ugaidi na misimamo mikali
inayoua maelfu ya watu wasio na hatia na kuwalazimisha mamilioni ya wengine
kuwa wakimbizi.
Katika upande mwingine
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza udharura wa kuchukuliwa hatua kali
zaidi za usalama nchini Niger. Ban Ki-moon ameitaka serikali ya Niamey
kuzidisha ulinzi kwenye kambi ya wakimbizi wa Mali kwa ajili ya kulinda
usalama wao.
Kwa sasa jeshi la
Niger limeanzisha operesheni kubwa ya anga na nchi kavu kwa ajili ya kuwasaka
wanachama wa kundi lililofanya mauaji ya wanajeshi hao ingawa hadi sasa
operesheni hiyo haijafanikiwa. Makundi kadhaa ya kigaidi yenye mfungamano na
kundi la al Qaida yamejikita katika eneo la kaskazini mwa Mali tangu miaka
mitano iliyopita na yamekuwa yakifanya mashambulizi na mauaji ya kutisha katika
eneo hilo na kwenye mpaka wa Mali na Niger. Shambulizi la sasa dhidi ya askari
wa Niger limefanyika baada ya serikali ya Niamey kurefusha kipindi cha hali ya
hatari katika maeneo ya kusini mashariki mwa nchi hiyo. Serikali ya Niger
imetangaza kuwa, sababu ya kurefusha hali hiyo ni mashambulizi yanayoendelea kufanywa
na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.
Katika mazingira haya
inaonekana kuwa, shambulizi lililofanywa na kundi la watu wasiojulikana dhidi
ya wanajeshi wa Niger ni tishio jingine kubwa kwa usalama wa nchi hiyo.
Kwa muda sasa nchi za
eneo la Ziwa Chad zimeanzisha mashambulizi ya kupambana na kundi la Boko Haram
na makundi mengine ya waasi lakini operesheni hiyo haijapata mafanikio ya
kuridhisha. Hii ni pamoja na kuwa, kuendelea kwa wimbi la wakimbizi wanaohama
kutoka maeneo ya vita na kwenda maeneo salama katika nchi jirani kama Niger ni
tatizo jingine linalozitatizo nchi hizo.
Shambulizi la kigaidi
la siku kadhaa zilizopita nchini Niger ni kengele nyingine ya hatari kubwa
ya harakari za kigaidi za makundi ya waasi katika eneo hilo la magharibi
mwa Afrika. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, kuna haja ya kuimarisha vikosi vya
jeshi katika maeneo ya mpakani na kushirikiana zaidi kwa ajili ya kung'oa
mizizi ya makundi hayo kupitia ratiba na mpango
maalumu.