Unatakiwa kutafuta kufurahi mara nyingi kadiri uwezavyo ili kukuongezea siku zako kuishi hapa duniani, Ndivyo wataalam wanavyosema, tabasamu lako linakuongezea muda zaidi wa kuendelea kuwa chini ya uso wa dunia, huzuni ni ishara ya kupunguza umri wa uhai wako. Turudi kwenye somo letu, leo mada inayohusu siri za kufurahia mapenzi, sasa twende kama ifuatavyo.
MFANYE NAMBA MOJA
Kuna baadhi ya marafiki wana fikra potofu (hasa wanaume),Hawa wanaamini kumpa mwanamke nafasi katika maisha ni kumfanya akukalie. Si kweli, Mwanamke unapompa nafasi ya kwanza, anaufurahia uhusiano wenu, Anajiona mwenye hadhi kubwa zaidi kwako, hutafuta njia za kukufanya umpende maradufu, kuliko kumuacha akijiona hana nafasi, Ongozana na mpenzi wako kwenye kumbi za burudani, mialiko ya sherehe mbalimbali, lakini pia mpe kipaumbele kwa kila kitu, Hili halihitaji elimu ya darasani, chunguza wenzako wanaowapa wenzi wao kipaumbele wanavyoishi, achana na mifumo ya kizamani, ukimpa mwenzako usawa anajiona hana nafasi kwako na thamani katika uhusiano mlionao.
MPE NAFASI
Hapa hakuna kitu kikubwa sana, ni kiasi cha kumpa nafasi katika mambo yako muhimu, Mathalani unataka kununua kiwanja Gongo la Mboto, Hata kama umeshaweka kila kitu sawa, lakini kumshirikisha tu, kutamfanya ajione mwenye nafasi kubwa kwako, Hili si kwa wanaume pekee, hata wanawake nao wanapaswa kutoa vipaumbele kwa wanaume zao. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuongeza ladha ya mapenzi kwa wapendanao, Inawezekana elimu hii imekupitia kushoto, hebu jaribu uone mafanikio yake,kumpa nafasi mwenzako katika mambo yako, tafsiri yake ni kumuamini na kumfanya azidi kujiamini kwako.
MTAMBULISHE
Mapenzi ya siri yana ukomo wake marafiki zangu. Ngoja niwaambie, unapokuwa unapenda mapenzi ya siri sana, unampa wakati mgumu mwenzako. Ni rahisi kufikiria kwamba, unafanya hivyo kwa kuwa ama hujiamini au una mtu mwingine. Weka mambo hadharani. Mtambulishe mwenzi wako kwa marafiki zako, Jiamini, unapokutana na mtu uliyesoma naye zamani au kuishi naye sehemu moja, mwambie kwamba uliyenaye ni mwenzako na unatarajia kuingia naye kwenye ndoa.
GUSIA MAMBO YA KIIMANI
Kuzungumzia mambo ya dini kulingana na imani yenu, kutamsogeza mwenzako kwenye ukweli kuwa una lengo naye la kuungana katika maisha ya ndoa. Angalizo kwako ni kwamba, wakati unamweleza hayo, iwe kweli yanatoka ndani ya moyo wako.
WAHUSISHE VIONGOZI WA DINI
Ikiwa uhusiano wenu umekomaa, unatakiwa kuwashirikisha viongozi wa dini. Angalia mazingira, unaweza kwenda naye, au kwenda mwenyewe na kuwaeleza nia yako. Waambie wakuombee au wawaombee ili uhusiano wenu uwe na nguvu, Kumbuka ndoa ni tendo la heri, hivyo shetani naye hutumia nafasi hiyo kuwaharibia! Kumuingiza Mungu katika uhusiano wenu kuna maana, mtakuwa katika ulinzi wenye nguvu zaidi, Yamkini pia, kama uliyenaye si chaguo kutoka kwa Muumba atamuengua mikononi mwako na kukupeleka palipo sahihi. Usiogope, nenda kaonane na viongozi wa dini na uwaeleze kinagaubaga.

KAMILISHA TARATIBU ZA KIFAMILIA/KIMILA
Ikiwa una uhakika kuwa mwenzako ndiye uliyemkusudia (zaidi kwa wanaume) wajulishe wazazi wako, kisha anza taratibu za kimila na kifamilia. Tuma wazee wapeleke posa, lipa mahari, halafu sasa anza kutimiza maagizo mengine yote utakayoagizwa.
Ni njia ya kuelekea kwenye ndoa. Uhusiano wenye baraka za wazazi, si tu kwamba unakuwa na nguvu, bali una radhi za wazazi wenu wa pande zote mbili, Je, kwa hali hiyo uhusiano wenu hautaimarika? Bila shaka utazidi kuchanua.

JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top