Kitu kibaya maishani ni kuonekana upo katika daraja la chini na mtu wa
kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna madhara makubwa. kila
mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata
heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Kitaalamu, hakuna
jambo ambalo hutokea maishani bila sababu maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako
au kwetu ndani ya jamii tunayoishi kunatokana na jinsi tunavyoenenda.
Hebu tuangalie njia za kukusaidia kurejesha heshima yako kwa
kuperuzi na wewe baadhi ya dokezo muhimu zinazoweza kukusaidia kujitambua na
kuweza kuyaepuka maisha ya kudharauliwa.
1. MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi
unavyoonekana. Muonekano ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa
ujumla. Hata siku moja hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata
kama ana kipaji kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa
mavazi na mwili huchangia mtu kudharauliwa katika jamii anayoishi. Linaweza
kuwa jambo dogo sana lakini ni moja kati ya sababu kubwa inayochangia
kuporomoka kwa thamani yako mbele ya wenzako.
2. KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala la uaminifu ni
pana, kuna uaminifu wa fedha, siri, dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema
kila unachoaminiwa lazima ukitunze kwani ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu
kuwa utashusha heshima yako.
3. UTENDAKAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote
heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku
wengine wakijiendekeza kwa tabia ya kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile
huchangia kubomoa heshima yako mbele ya jamii. Fanya kazi usiishi bila
kujishughulisha.
4. Mazungumzo
Hapa naomba nieleweke
kuwa unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli
zisizo na busara zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na
mantiki huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi.
Biblia inasema penye wingi wa maneno hapakosi uovu.
5. KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za
kuahidi mambo halafu unashindwa kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi
mbaya ya kutunza heshima yako katika jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi
kuliko kuahidi na kutotimiza.
6. SIFA ZISIZO NA MAANA
Nakumbuka msemo mmoja
kutoka kwa mwandishi mwandamizi aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha,
marehemu Adolf Balingilaki, ambao unasema kwamba:“Ukitafuta heshima kwa gharama
ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha
nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako
kuwa ya kujiinua, watu watakudharau.
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv