Mzazi anaporudi nyumbani jioni, kwa mfano, watoto hutarajia
pipi hata kama hawajafanya chochote. Lakini kadri mtoto anapoendelea kukua,
mtazamo wa zawadi kama haki hupungua. Mtoto huanza kufikiria zawadi kama
matokeo ya kufanya kile kinachotarajiwa na mzazi. Watoto wanapenda zawadi.
Katika umri mdogo, mtoto huchukulia zawadi kama
haki ya kupata kila akipendacho kwa wakati wowote. Mtoto anapofaulu mtihani, anatarajia
kitu. Unapompa kile anachokitarajia, anajenga hamasa na motisha ya kutia bidii
zaidi masomoni.
Aidha, uzito wa zawadi kwa mtoto hutegemea na wakati. Zipo nyakati ambazo
zawadi hubeba maana zaidi kwa watoto kuliko wakati mwingine.katika familia nyingi, msimu wa sikukuu unapokaribia watoto
hutarajia zawadi zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hawezi kuelewa pale
inapotokea mzazi anashindwa kutoa zawadi inayotarajiwa.
Zawadi ni chochote kile anachopewa
mtoto kwa minajili ya kukuza uhusiano wake na mzazi na hata kujenga motisha ya
kuimarisha tabia njema.Hata hivyo, pamoja na manufaa hayo ya zawadi, utoaji holela wa zawadi
unaweza kutengeneza matatizo ya kitabia.
leo tunajadili mambo matano ya kuzingatia unapomzawadia
mwanao.
kwanza kipi ni zawadi kwa mwanao
Siyo kila kitu unachompa mtoto kinaweza kutafsirika kama zawadi kwake. Ili
zawadi yako iwe na maana, ni muhimu kumfahamu mtoto vizuri kujua mambo yepi
anayapenda zaidi.
Katika
umri mdogo, watoto wengi hupenda vitu vitamu. Unapowaletea pipi, keki, biskuti
unakuwa umewaweza. Lakini wanapokua, wanajenga matarajio mengine. Ni muhimu
kuyaelewa.
Hakikisha zawadi inaendana na kile anachokipenda mtoto. Kila mtoto ana
mambo anayopenda kuyafanya katika muda wake binafsi. Kama mwanao anapenda
kuchora, kwa mfano, inaleta maana kumletea zawadi ya rangi badala ya michezo ya
kidijitali hata kama kwako michezo hiyo inafurahisha zaidi.
Kadhalika, uzito wa zawadi kwa mtoto pia hutegemea nyakati. Katika sherehe
ya kuzaliwa, kwa mfano, mtoto anakuwa na matarajio tofauti na yale anayokuwa
nayo wakati mwingine. Unapofanya kama anavyotarajia, ni rahisi kuchukulia kwa
uzito na hivyo akajisikia vizuri.
Unatakiwa kuifanya zawadi iwe adimu
Zawadi inayotolewa mara kwa mara inakuza matarajio. Mtoto anapojua kuwa
lazima atapata zawadi kila unaporudi nyumbani, hujenga mazoea ya zawadi. Ili
muendelee kuwa marafiki, utalazimika kuendelea kwenda na zawadi kila siku.
Mazoea
haya yanajenga tabia ya utegemezi wa zawadi. Inapotokea umeshindwa kumpelekea
zawadi kama alivyotarajia, uhusiano wenu unaweza kuzorota. Katika mazingira
haya, maana ya zawadi inapotea kwa sababu mtoto anakuwa amejenga matarajio
kwenye zawadi.
Sambamba na hilo, ni muhimu zawadi iwe ndogo. Hakuna sababu ya kutoa zawadi
kubwa itakayokugharimu pale itakapozoeleka. Zawadi ndogo inayoambatana na
uhusiano mzuri na mwanao, inaleta mantiki kuliko ukubwa wa zawadi.
Pia, badala ya kujenga mazoea ya kutoa zawadi ya vitu, unaweza kuanzisha
mazoea ya kutoa zawadi zisizonunulika. Kwa mfano, unaweza kumpa mtoto pongezi
za mdomo zinazoonyesha kutambua kilichofanywa; kuwa na wakati mzuri na mwanao
nje na nyumbani; kumkumbatia kwa upendo; kumruhusu kuwa na muda na rafiki zake
na matendo kama hayo yanayoimarisha uhusiano wenu.
Ni vyema Ifahamike imetolewa kwa sababu gani
Lengo la zawadi ni kukuza tabia inayotarajiwa. Unapompa mwanao zawadi
kutambua tabia njema aliyoionyesha unamjengea ari ya kufanya vizuri zaidi.
Hakikisha mwanao anajua kwa nini umempa zawadi. Zawadi isiyojulikana ina
malengo gani haiwezi kumsaidia mtoto.
Kama mwanao amefanya vizuri shuleni na unadhani anastahili motisha, mpe
zawadi inayoambatana na ufafanuzi. Kama mwanao ameonyesha jitihada za kukuza
tabia fulani njema, mpe zawadi kwa maelezo.
Unapohakikisha kuwa mwanao anafahamu kwa nini umempa zawadi, utamfanya awe
na ari ya kuendelea kuonyesha tabia hiyo kwa matarajio ya kupata zawadi zaidi
kwa wakati mwingine.
Inatakiwa iwe na manufaa kwa mtoto
Mpe mtoto zawadi yenye manufaa na itakayomsaidia kujifunza. Kwa mfano,
vifaa vya shule kama kalamu, rangi za kuchorea, vitabu, vifaa vya michezo,
madaftari, CD za elimu vitakavyomsaidia kujenga uelewa na kukuza vipaji vyake.
Fikiria kumpa mtoto kiasi kidogo cha fedha taslimu atakachowajibika
kukitunza. Ingawa jambo hili linahitaji kufanyika kwa tahadhari, lakini
humsaidia mtoto kujenga tabia ya kuwa na nidhamu ya fedha mapema.
Unatakiwa uitoe wakati usiotarajiwa
Upo ukweli wa kisayansi kuwa wakati tabia mpya inajengwa, unalazimika
kuhakikisha kuwa zawadi yako inatolewa kila mara tabia hiyo inapojitokeza. Kwa
kufanya hivyo, unajenga motisha inayosaidia kumsukuma mtoto kufanya kile
kinachotarajiwa.
Hata hivyo, baada ya mtoto kujifunza tabia hiyo mpya, unahitaji kubadili
utaratibu. Ukiendelea kuitoa kila mtoto anapoonyesha tabia hiyo, zawadi kujenga
utegemezi. Badala ya mtoto kujifunza tabia husika, anajifunza kungoja zawadi.
Inapokosekana, tabia iliyojengwa hupotea mara moja.
Ni vizuri kuhakikisha kuwa zawadi haifahamiki itatolewa lini. Hakuna sababu
ya kumjengea mtoto mazoea ya kupata zawadi nyakati za sikukuu. Kama anahitaji
mavazi, mnunulie wakati mwingine wowote. Ukifanya hivyo, hutadaiwa zawadi
nyakati za sikukuu zinapowadia.
MWANANCHI..
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv