Pamoja na mwamko mkubwa wa kushirikiana katika kazi za nyumbani kati ya mama na baba, bado mwanamke ana dhima kubwa kuliko mwanaume. Nakumbuka mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Magreth Thacher aliwahi kukiri hadharani kuwa pamoja na majukumu makubwa ya kuendesha nchi, alipokuwa nyumbani alikuwa akifanya kazi za nyumbani. Hata, alikuwa akimpikia na kumwandalia mumewe chakula.
Wale wanawake walikubaliana kuwa ulimwengu wa sasa umebadilika sana kwa pilikapilika na misukosuko. Siyo kama ule wa zamani ambapo mama zetu na bibi zetu waliweza kulea watoto hadi sita, wakapika vyakula vitamu, wakafanya usafi wa nyumba, wakafua marundo ya nguo kwa mikono yao, wakasenya kuni na kuteka maji kwa kichwa.
Pamoja na yote hayo waliweza kutengeneza vifaa vya nyumbani kama kufinyanga vyungu, kusuka mikeka na kujenga vihenge vya kuhifadhia nafaka. Vilevile waliweza kushiriki katika shughuli za kijamii na burudani kama kucheza ngoma.
Lakini katika maisha ya leo, ambapo wote mume na mke wanafanya kazi na wana watoto kadhaa wanaowalea wenye ratiba yao pekee ya mambo ya shule na nyumbani. Kutokana na yote haya hawana budi kukabiliana na maisha ya leo yenye changamoto nyingi. Wanandoa wote hususan mwanamke atagundua kuwa katika maisha yake anapungukiwa muda wa kutosha kufanya mambo yote yanayompasa. Siku ina saa 24 na haziwezi kuongezeka. Tena, karibu saa nane za muda huo hutumika kwa usingizi.
Hizo  saa 16 zinazobaki huwa haiwezekani kutumika zote kwa kazi. Utafiti umebainisha kuwa kwa wastani mtu hupoteza karibu miaka tisa ya uhai wake kwa kufanya shughuli zisizo na tija yoyote.
Shughuli hizo ni kama kukaa kwenye foleni benki, posta na kwengineko; kusimama barabarani kungojea taa za waenda kwa miguu, kutafuta watu kwenye simu, kwenye mikutano isiyo na tija na mengine kadhaa wa kadhaa ya jinsi hii.
Leo tuangazie baadhi ya mambo yanayoweza kumsaidia mwanamke kujipanga kuzifanya kazi kwa utaratibu ulio sahihi zaidi na kuepuka matumizi mabaya ya muda mchache alionao katika siku.
Kuweka malengo na vipaumbele
Hii ni hatua ya kwanza kabisa ambayo mwanamke anapaswa kuitumia katika kufanya kazi huku akiyafanya maisha yake yawe ya raha. Akumbuke kuwa mambo anayopaswa kuyafanya nyumbani na kwa familia yake ni mengi sana na hawezi kuyamaliza yote.
Hivyo anatakiwa kila siku kufikiria mambo yote unayotakiwa kuyafanya. Kisha ujiulize yapi yanaweza kusubiri na yapi hayawezi kusubiri. Hatimaye aorodheshe yale anayopaswa kuyatimiza katika siku fulani na ayapange kufuatana na umuhimu. Ayatekeleze kwa kuzingatia vipaumbele katika siku juma na hata mwezi.
Kutumia vifaa vya kurahisisha kazi
Katika ulimwengu wa leo wa sayansi na teknolojia kuna zana na vifaa vingi vinavyoweza kumsaidia mwanamke katika kudhibiti utekelezaji wa mangilio wa kazi, kutumia vyema wakati na kurahisisha kazi zake. Baadhi ya zana hizo ni hizi zifuatazo:-
• Kulenda: Kalenda ya ukutani au mezani ni zana muhimu katika kumkumbusha mambo muhimu unayotakiwa kufanya katika mwezi. Mwanamke aliye makini katika shughuli zake huweza hata kuwa na kalenda ndogo katika mkoba wake. Kalenda zake zitakuwa zimechafuka kwa kuziwekea maelezo yake.
• Saa: Saa ya ukutani na mkononi ni rafiki wa mwanamke anayejali wakati na aliye makini katika kazi zake. Watu wengi husahau kuwa ni muhimu kuwa na saa mbele yake anayoitazama kwa urahisi wakati wote ili kuchunga matumizi ya muda. Licha ya kuwa saa kazini na nyumbani ni muhimu mwanamke awe na saa hata jikoni.
• Kijitabu cha kumbukumbu: Mwanamke wa kisasa analazimika kuwa na kijitabu kidogo cha kuandika mambo mbalimbali kama yale anayotakiwa kuyafanya katika siku. Vijitabu hivi huwa na tarehe. Jambo alilopanga kulifanya siku fulani asipolitekeleza siku alihamishie katika ukurasa wa siku inayofuata. Jambo ambalo limehamishwa zaidi ya siku mbili aanze kulindika kwa wino mwekundu ili kumtahadharisha kuwa limechelewa kutekelezwa.
• Vikaratasi vya kubandika kwa ajili ya kumbukumbu: Katika maduka ya steshenari huuzwa vipande vidogo vidogo vya karatasi vyenye gundi upande mmoja vinavyoweza kubandikwa katika sehemu mbalimbali. Hivi vinatumika kwa kuandika mambo ambayo mtu amepanga kuyafanya kisha anakibandika mahali ambapo atakiona wakati wote ili kulikumbuka jambo hilo.
Kwa kuwa huwa vina rangi mbalimbali mwanamke anaweza kuamua rangi fulani kwa kazi za aina moja na rangi nyingine kwa kazi za aina nyingine. Hivi anaweza kuvibandika sehemu mbalimbali ili kumkumbusha kama vile ukutani, kwenye friji, gari na kwingineko.
• Kikokotozi: Hiki ni kimashine cha kufanya hesabu ambacho ni muhimu mwanamke wa kisasa awe nacho anapoandaa bajeti ya matumizi ama anapokwenda kununua vitu dukani. Ahakikishe kila wakati anacho katika mkoba. Kwa bahati siku hizi simu za mkononi zina vikokotozi.
• Mafaili ya kutunzia nyaraka: Hivi ni vifaa muhimu sana kwa mwanamke wa kisasa. Atakuwa na faili kwa nyaraka mbalimbali muhimu kama vile bili za maji, umeme, uzoaji wa takataka, kodi ya nyumba na vinginevyo. Pia kuna nyaraka nyingne muhimu kama hati za kuzaliwa watoto wake, mkataba wa bima ya afya, stakabadhi za ununuzi wa vitu vikuu nyumbani kama TV, Friji, Radio, Jiko n.k.
mwananchi
Zipo nyingi ila endelea kufuatilia edonetz niaendelea kukuletea mada hii. 
JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv


 
Top