Wapo watu maisha yao ya kazi yamejaa wasiwasi. Wanapoingia kazini hawajiamiani. Wapo wanaofikia hatua ya maradhi ya shinikizo la damu kwa sababu ya aina ya mabosi walionao kazini.
Wengine wapo kazini kwa kuvumilia kuliko kupenda wanachofanya. Hawa ni wale wanaofanya kazi kwa sababu ya mshahara. Hapendi alipo lakini hana jinsi, maana kipato anachoingiza ndicho kinampa uwezo wa kutatua shida zake za kimaisha.
Kwa nini usifurahie kuwapo sehemu inayokupa riziki yako? Hupaswi kuamka asubuhi umekunja ndita wakati ukielekea kazini. Haitakiwi njia nzima uwe unaomba ukute bosi wako hajafika.
Usiishi kama panya, kwamba wao hutamba na kufanya safari nyingi ndani ya nyumba pale paka anapokuwa hayupo.
Hutakiwi kuwa na furaha pale bosi wako asipokuwapo. Tabasamu na furaha yako vinapaswa kuwapo muda wote, tena vichanue mbele ya bosi wako.
Je, bosi wako ni mkorofi na anakufanya kila ukimuona utetemeke? Siyo shida, jukumu la kumtuliza ni lako mwenyewe. Njia za kumfanya azungumze na wewe kwa upole badala ya ukali zipo ndani ya uwezo wako.
Eneo la kutambua sababu ya wewe kuajiriwa ni muhimu zaidi. Maana kama hutambui upo kazini kwa ajili gani, hata ukaririshwe mbinu milioni bado hazitakusaidia. Kutambua humaanisha akili inafanya kazi sawasawa, inajielewa. Baada ya hapo zipo silaha nne za kushika.
Nidhamu
Utii wa kila kitu kazini utakufanya usimwogope bosi wako. Hapa sizungumzii utii wa woga au nidhamu ya woga kama inavyofahamika kwa wengi. Nidhamu ninayozungumzia hapa ni ile ya kuhakikisha kila kitu kinakuwa kwenye mpangilio wake.
Bosi wako ni mkorofi, vilevile ni msema ovyo na anapenda kukaripia. Nidhamu yako ya kufanya mambo yako kwa mpangilio, itamnyima sababu ya kufoka. Akishazoea kutokufokea moja kwa moja ndani yake kunakuwa na zuio la ukali juu yako.
Kisaikolojia, hali ya kufoka haiji mara moja, bali hufuata baada ya mazoea. Huwezi kuwa mfanyakazi mgeni siku ya kwanza tu bosi wako akafoka na kukukaripia. Vipo vitendo hutengeneza mfikie hali hiyo.
Nidhamu yako itadhibiti vishawishi vya kufokeana.
Watu wazima wanapofokeana, tafsiri yake ya kisaikolojia ni kuwa kuna nyuzi za kuheshimiana zimekatika. Usikubali kukosewa heshima na kudhalilishwa kwa kufokewa mbele za watu kazini. Kumbuka kuna aina kadhaa za nidhamu kama inavyoanishwa hapa chini.
Nidhamu ya kuwahi kazini; fika muda ambao umepangwa au kabla. Mara nyingi suala la kuwahi lina changamoto zake lakini kwa vile unalinda heshima, wahi kila siku. Mnyime bosi wako sababu ya kuzungumza kuhusu mahudhurio.
Nidhamu ya utendaji; hakikisha majukumu yako yanatimia kulingana na muda. Kila kazi zako zinapouliziwa ziwe tayari au zimefika hatua nzuri.
Nidhamu ya usafi; usafi wako binafsi na ule wa kazi yako ni muhimu. Uchafu utasababisha nyuzi za kuheshimiana zikatike kisha iwe mwanzo wa bosi wako kukufokea.
Nidhamu ya mawasiliano; wasiliana vizuri na bosi wako pamoja na wafanyakazi wenzako. Eneo la mawasiliano likilega litakutengenezea kasoro. Fahamu kuwa njia kuu ya kummudu bosi wako mkorofi ni kumfanya asikuangalie kwa jicho hasi.
Juhudi
Lazima ujipambanue kama mchapakazi. Uvivu utakupa wakati mgumu mbele ya bosi mkorofi. Fanya kazi kwa bidii na juhudi yako ionekane kazini. Unapomaliza majukumu yako ya siku, si vibaya ukawasaidia na wenzako muda unapokuruhusu.
Ikitokea kazi mpya na bosi wako anapita akiuliza nani anaweza kuifanya, nyoosha mkono na umwambie akuachie wewe uifanye.
Juhudi na moyo wako wa kujitolea kazini vitamfanya bosi wako abadilike kutoka kuwa mkali hadi kuwa mpole na mwenye upendo.
Ukiwa na juhudi kazini utamfanya bosi wako apende kukuona. Aone ulazima wa wewe kuwapo. Mara nyingi bosi anapokufokea, huo ni ujumbe kuwa hata usipokuwapo yeye hababaiki.
Maarifa
Jibiidishe kuongeza maarifa ya kazi yako ili unapoifanya matokeo yawe tofauti na wengine. Hakikisha viwango vya ufanisi wako vinakuwa bora, hivyo kumlazimisha bosi wako akuone ni muhimu.
Ukiwa na maarifa ya kutosha kwenye kazi yako, utaifanya kazi yako kwa weledi. Boresha maarifa yako ya darasani, boresha zaidi kwa vitendo. Ujuzi wako utamfanya bosi wako aone usipokuwapo mambo mengi yataharibika.
Ukiwa na maarifa ya kutengeneza matokeo bora kwenye kazi, maana yake unakuwa kiungo nyeti kazini. Unapokuwa kiungo nyeti, wewe mwenyewe unajisikia upo salama. Huwezi kuishi kwa wasiwasi wa kufukuzwa kazi wakati wowote au kukaripiwa.
Unapokuwa na maarifa ya kutosha, utashangaa bosi wako mkorofi anafokea watu wengine halafu anakwita ofisini kwake au anakuja kwako mjadili kazi. Hivyo basi, kila siku jitahidi uongeze maarifa kwenye kazi yako ili uonekane mpya wakati wote.
Kujiamini
Nidhamu unayo, unafanya kazi kwa bidii na una maarifa ya kutosha juu ya kazi yako, sasa wasiwasi wa nini? Unapojiamini unaongeza thamani yako kazini na ukiwa muoga utachukuliwa kama ulivyo.
Mfanyakazi mwenye kujiamini na akawa anaifanya kazi yake vizuri, humfanya bosi mkorofi ajiulize namna ya kumuingia. Ukiwa muoga, muda wa kazi unaweza kutimia lakini bosi akakwambia ubaki.Anajisikia kutokana na woga wako.
Badala ya kuwa na woga bosi wako anapokupigia simu au kukuulizia, wewe mpigie au mfuate ofisini kwake na mzungumze kuhusu kazi. Ukikutana naye msalimie kwa kumpa mkono. Hakikisha unajiamini bila kupunguza japo nukta.
JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top