Watoto wadogo kunyonya kidole kutokana na mahitaji
ya kimwili na kisaikolojia. Mtoto huanza kunyonya kidole endapo hapati maziwa
ya kutosha. Mara nyingine husababishwa na matatizo ya kihisia.
Kwa mtoto, kunyonya kidole ni namna ya kujifariji.
Mtoto asipotosheka kila anaponyonya maziwa huanza kunyonya kidole ambacho
humfanya apunguze njaa. Kisaikolojia; hujibembeleza na kujisikia salama.
Mara nyingi mtoto ataacha kunyonya kidole akiwa na
umri kati ya miaka mitatu mpaka sita ingawa wengine huendelea hadi ukubwani.
Inasemekana kuwa tabia hii huanzia tumboni baada ya
wiki 13 za ujauzito na huendelea mpaka mtoto anapozaliwa ingawa wazazi wengi
hugundua hilo mtoto anapofikisha umri wa miezi miwili mpaka mitatu.
Zipo faida zilizothibitika za watoto kunyonya
kidole. Nyingine zinaendelea kuchunguzwa. Baadhi ya watafiti wanadai unyonyaji
huo huimarisha kinga ya mwili. Watafiti hao wanadai unyonyaji wa dole gumba na
ung’ataji wa kucha husaidia kuzuia mzio (allergy).
Hasara
Kama ilivyo kwa masuala mengine yoyote, hili nalo
lina hasara zake. Zipo zitokanazo na mtazamo na imani za jamii husika na zile
za kimuonekano.
Kwenye jamii zilizopo, baadhi ya watu huamini mtoto
anayenyonya kidole anajipunguzia uwezo wa kuzingatia masomo hivyo kuwa mjinga
jambo ambalo kitaalamu halijathibitika.
Upo uwezekano wa mdomo hasa kuathirika. Inaelezwa
kuwa ‘lips’ zinaweza kulegea
kutokana na uzito wa kidole sambamba na mtoto kuchelewa kuwa na ufahamu
kutokana hutumia muda mwingi kunyonya kidole. Wazazi wanashauri kuwa macho ili
kunusuru hali hii.
Endapo mtoto ataendelea kunyonya hata akiwa na umri
mkubwa kidogo inaweza kusababisha meno kutojipanga vizuri kwenye fizi.
Madaktari wa kinywa wamehusisha mpangilio mbaya wa meno na kunyonya kidole hasa
gumba kwani meno husukumwa kwenda mbele au kujipanga vibaya na hivyo kuathiri
muonekano wa mhusika.
Kunyonya kidole siyo hatari ikiwa mtoto ataacha kabla
ya miaka mitano. Kama mtoto atashindwa kuacha kunyonya kidole mpaka baada ya
umri huo kuna uwezekanao mkubwa wa meno yake kutojipanga vizuri na kuota yakiwa
yamebebana au kuwa na meno yasiyokutana.
Watoto wanaonyonya kidole baada ya miaka minne au
mitano wana hatari ya kupata tatizo hili hivyo kuathiri muonekano wao wa sura
na hata matatizo ya kuongea vizuri.
Hii huweza kutokea kutokana na kulegea kwa lips
ambazo ni muhimu kwa matamshi ya baadhi ya maneno. Meno yaliyokosa nafasi au
yenye nafasi kubwa nayo yana athari kwenyemmatamshi. Kutokana na kunyonya huko
mtoto atapata tatizo la matamshi na viungo vya mdomo mfano ulimi kutoka nje
wakati wa kuongea.
Inategemea na ukubwa wa athari. Kama mpangilio
haujawa mkubwa sana mpangilio mbaya huweza kujirekebisha wenyewe iwapo mtoto
ataacha kunyonya kidole. Kwa wale wanaopitiliza wanahitaji huduma za mtaalamu
wa meno (orthodontist) kufanya marekebisho.
Ushauri
Inashauriwa kutomkataza mtoto kunyonya kidole akiwa
chini ya miaka minne au mitano isipokuwa kama kuna tatizo linalojitokeza au
mtoto akianza ghafla kufanya hivyo baada ya miezi 10 tangu azaliwe na
ikiambatana na kuvuta nywele.
Ili kupunguza uwezekano huo, mama anayenyonyesha
anapaswa kula vyakula vyenye lishe kamili vitakavyosaidia mwili kutengeneza
maziwa ya kutosha kumnyonyesha na kumshibisha mtoto kila wakati hivyo
kumuepusha kunyonya kidole.
Kwa mtoto anayenyonya, wazazi au walezi wanapaswa
kumueleza kwa upole wakitumia lugha laini ikibidi kumuahidi zawadi nzuri ili
akubali kuacha kunyonya kidole.
Kumuanzisha shule ni njia nyingine inayoweza
kumsaidia mtoto kuacha kunyonya kidole. Shule kutamfanya aone aibu na kuacha
hasa atakapokuwa anataniwa na wenzake anaosoma na kucheza nao.
Njia mbadala pia zinaweza zikatumika. Hizi
zitamsaidia kuacha mapema zaidi. Kupaka pilipili vidole vyake ili akinyonya
awashwe na ukali atakaokutana nao itamfanya asirudie tena kufanya hivyo ingawa
kutakuwa na jukumu la kumbeleza kila atakapokuwa analia baada ya kunyonya
kidole.
Kushiriki michezo inayoshughulisha mikono kwa muda
mwingi ni njia nyingine ya kufanikisha suala hili. Unaweza ukampa midoli (wanasesere),
au acheze na wenzake ili mradi viganja vyake viwe na shughuli ya kufanya na
kumnyima nafasi ya kunyonya kidole.
Pia, unaweza kumnunulia nyonyo za plastiki ili umpe
anyonye badala ya kidole. Hii itamfanya asipate muda wa kuzoea kunyonya kidole.
Kuwavalisha watoto mipira ya mikono au viganja (gloves)
na kuwafanya washindwe kunyonya vidole.
Iwapo vyote hivyo vitashindikana basi mzazi au
mlezi asisite kuwaona madaktari wa afya ya meno na kinywa kwa msaada zaidi.
Source mwananch;
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv