Ukosefu wa ajira
huwakatisha watu tamaa na hata kuwafanya washawishike kujiunga kwenye vitendo
visivyofaa, maana hapo kabla walikuwa wakiamini baada ya masomo kupata kazi ni
mteremko Msongo wa mawazo au kukata tamaa, haviwezi kukusaidia kukuondoa kwenye
hali uliyonayo.
Huna ajira hilo ni sawa
lakini unapaswa kutambua kuwa hiyo hali ni ya kupita. Baki na matumaini kuwa utapata
kazi nzuri kulingana na vigezo vyako vya kitaaluma na ujuzi mzuri ulionao.
Endelea kujiamini kuwa wewe ni mtu bora kikazi ambaye muda ukifika utauonyesha
na kutoa kila ulichonacho.
Kuna kanuni tatu ambazo
unapaswa kuzizingatia unapokuwa kwenye changamoto ya kukosa ajira, kwanza
ni kujijali. Jipende
na ujijali kila wakati. Usiyafanye
macho ya pembeni yakuone unadhoofika au unakuwa mchafu, kisa huna kazi!
Vaa vizuri na uonekane nadhifu, kwani usafi wako unaweza
kumvutia mtoa ajira.
Kanuni ya pili ni kutabasamu. Usishike tama, onekana na
tabasamu lako kila wakati. Ukitabasamu mbele za watu na wenyewe watatabasamu.
Kanuni ya tatu na mwisho ni kuchangamka. Ukikutana na watu
changamka na uonyeshe upo vizuri kiakili na kimwili. Uchangamfu wako hutoa
picha kwamba afya yako ya mwili na akili vipo imara. Baada ya hapo zingatia
mambo matano yafuatayo.
Jiweke
sokoni
Andaa wasifu wako (CV)
ambayo umeuandika vizuri kisha uwasilishe kwenye maeneo unayoona yanafaa au
yale ambayo ungependa upate kazi. Usikae tu kwa sababu umeambiwa ajira hakuna.
Hapana, jiweke sokoni ujulikane.
Kimsingi, unatakiwa
urahisishe upatikanaji wako. Simu yako iwe wazi ili ukipigiwa upatikane. Wengi
hukosa ajira kwa sababu ya kuweka namba za simu zisizo na uhakika, anapigiwa
hapatikani. Wenye kutafuta ajira ni wengi, aliye rahisi kupatikana ndiye hupewa
kipaumbele.
Jiongezee thamani
Kipindi ambacho huna ajira,
unaweza kukitumia kujiongezea thamani kwa kusoma kozi tofauti zenye kuongeza
uzito wa ujuzi au taaluma uliyonayo. Lazima ufahamu kuwa wanaoshinda kwa
urahisi katika soko la ajira ni wale wenye sifa za ziada.
Tumia muda wako kusoma
lugha za kimataifa. Siku ukiingia kwenye mchakato wa ajira, utajikuta ni bora
zaidi kwa sababu unaweza kuzungumza na kuandika kwa kutumia lugha nyingi kuliko
wenzako.
Jiongeze thamani kwa kusoma
zaidi kompyuta. Ulimwengu wa teknolojia huu; fikiria unaomba kazi ya uofisa
mauzo, pamoja na kuwa na sifa zinazotosha kupata kazi hiyo, unakuwa na nyongeza
ya kujua kompyuta kwa sababu ulisoma pia Tehama.
Nenda chuo cha udereva na
ukishafuzu fanya mchakato upate leseni. Thamani yako inaweza kuongezwa na hilo,
kwamba wenzako walioomba watahitaji dereva kutimiza majukumu yao, wakati wewe unaweza
kujiendesha mwenyewe kama utapewa gari na ofisi.
Jitangaze kisasa
Tambua ulimwengu uliopo
kisha utumie urahisi wa kiteknolojia kujitangaza. Wewe ni mhandisi, hakikisha
unafungua blogu na kuwa na akaunti za mitandao ya kijamii ambayo utaitumia
kuandika na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu eneo lako.
Utakapokuwa unaandika
utawafanya watu wengi zaidi wakuone. Matokeo yake utaonwa na waajiri. Jinsi
ambavyo unajipambanua kwa kueleza kasoro za kiutendaji katika eneo lako na
kutoa mwanga wa kile ambacho kinapaswa kufanyika, itawafanya waajiri wakuone
wewe ni bidhaa bora kuwa nayo.
Unaweza kujitangaza pia kwa
kuomba kurasa kwenye magazeti. Kuliko kukaa tu bila kazi, hebu kile ambacho
unacho kichwani kiweke kwenye maandishi kupitia magazeti. Omba kuhojiwa redioni
na kwenye televisheni, huko ndiko kujitangaza kisasa.
Inawezekana waajiri
hawasomi blog yako, hawapitii mitandao ya kijamii wakaona kile ambacho umekuwa
ukikitoa lakini siyo tatizo. Andaa vipande vya video au maandiko yako na
kupeleka kwa waajiri. Hapo unakuwa unajiweka katika hali inayoutangulia wakati
uliopo.
Jitolee kufanya kazi
Omba kazi ya kujitolea
ukiwa unajiamini kuwa baada ya muda wewe ni rasilimali inayohitajika. Unapokuwa
unajitolea hakikisha unatoa kila ulichonacho ili kuwapa hamu waajiri waone
ulazima wa kukaa na wewe mezani na kujadiliana jinsi ya kufanya kazi pamoja kwa
mkataba wa muda mrefu.
Unaweza kujitolea pia kwa
kufundisha. Unapokuwa unaingia darasani kufundisha inakusaidia kuendelea
kutunza kile ulichonacho na kujiogezea. Kimsingi, kufanya kazi kwa kujitolea
kuna maana kubwa na kunakufanya uwepo kwenye mzunguko wa ajira.
Iwe kujitolea kufanya kazi
mahali au kwa kufundisha, muhimu ni kuwa inakuongezea thamani kwenye CV yako. Inakupa ile hadhi ya uzoefu
ambayo hutakiwa na waajiri wengi.
Watu ambao wametoka chuo na
hawajawahi kufanya kazi hiyo mahali popote huogopwa na waajiri, kwa maana
huonekana huingia kazini kama wanafunzi wenye kuhitaji maelekezo na mafunzo
mengi ili waijue kazi.
Unaweza kujiajiri
Usikae tu damu yako
italala, wakati ambao upo na ari ya kufanya kazi lakini ajira hakuna, hebu
angalia jinsi ya kujitengenezea ajira. Umesomea masuala ya uongozi wa biashara,
unaweza kujiajiri kama mshauri wa usimamizi wa biashara.
Angalia ulichosomea, kisha
kitengenezee ajira binafsi au hata kuajiri wengine. Siy vibaya ukajiajiri
kwenye mambo mengine ambayo hata hukusomea, ilimradi unaona urahisi kuanza na
kufanikiwa. Usibweteke kwa kukosa ajira, amka na uonyeshe matokeo.
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv