Leo tuzungumzie wanawake ambao ni majanga na ukijichanganya ukaingia nao kwenye maisha ya ndoa, inakula kwako.

Anaona unamsaliti kila mara

Huku kunatokana na kutokujiamini tu. Ukioa mwanamke ambaye kila wakati unapokuwa mbali naye anahisi unamsaliti, huyo hakuamini na kamwe hamuwezi kudumu. Mara kadhaa mtakuwa mkigombana akihisi una mwingine kumbe hakuna ukweli katika hilo.

Asiyeridhika na penzi unalompa
Wapo wanawake ambao wewe unaweza kujitahidi kumpatia mapenzi kadiri unavyoweza lakini yeye hatosheki. Anakuchukulia wewe ni dhaifu sana na wakati mwingine kuhisi yupo mwingine anayeweza kumpa zaidi ya kile unachompa, huyu ni tatizo.

Anahisi amekosea kuwa na wewe
Wapo wanawake ambao wanapoingia kwenye ndoa baada ya muda wanahisi wamekosea kuolewa na mwanaume huyo. Unakuta mke wa mtu anahisi fulani ambaye zamani alikuwa kwenye uhusiano naye angekuwa sahihi zaidi baada ya kuona upungufu fulani kwa huyo aliyemuoa.

Wivu kupindukia
Hatukatai, wivu ni muhimu sana kwenye suala la mapenzi lakini kuna ule wivu uliopindukia kiasi cha kuwa kero. Walio kwenye ndoa wananielewa namaanisha nini.
Kwa kifupi mtu mwenye mapenzi ya dhati na mwenziye lazima awe na wivu lakini ukiwa na ule wa kupinduki ni tatizo linaloweza kuitibua ndoa.

Yuko kimasilahi zaidi
Kuna wanawake ambao ukiwaoa wanakuwa na furaha na wewe ukiwa unazo tu, ukiishiwa wanaanza kununa na kuleta visirani vya hapa na pale. Hawa ni tatizo, mwanamke wa kweli ni yule anayeridhika kuwa na wewe kwenye shida na raha

Hapendi ndugu zako
Waswahili wanasema ukipenda boga, penda na ua lake. Kama utatokea kuoa mwanamke ambaye anakupenda wewe tu lakini akija ndugu, rafiki au mtu mwingine wa karibu yako anabadilika, huyo ana matatizo kwani atakufanya utengwe na jamii yako.

Yuko tayari kuachana na wewe

Hivi hujawahi kumsikia mke wa mtu akimwambia mumewe; ‘Kama vipi tuachane, kwanza kwetu sijafukuzwa na nilikuwa nakula, nalala, navaa.” Mwanamke anayeweza kumtamkia mume wake maneno haya, huyo si mke na kamwe hawezi kukufanya uwe na furaha.

Anataka awe na sauti
Mwanaume siku zote atabaki kuwa kiongozi wa familia lakini wapo baadhi ya wanawake hawataki kukubaliana katika hilo. Wengi wanalazimisha usawa na wengine wakitaka wao ndiyo wawe na sauti kuliko wanaume zao.

Anajali mafanikio binafsi
Siku zote wawili waliotokea kupendana wakioana wanakuwa mwili mmoja hivyo lazima watakuwa wanawaza na kufanya maamuzi pamoja.
Ogopa sana mwanamke anayependa kutumia kipato chake kufanya mambo binafsi tena kwa siri. Kwa mfano kusaidia kwao, kujenga nyumba kwao, kuanzisha miradi yake bila kukushirikisha.

Eti akizaa utamzeesha
Hili kwa wale wanaopenda kuoa masistaduu. Wapo ambao wakitajiwa suala la kuzaa mara baada ya kuingia kwenye ndoa wanagoma wakidai eti watazeeshwa hivyo waachwe kwanza wale ujana. Wakati huo unaweza kukuta mwanaume anataka mtoto ili apate ile heshima, mke anagoma kwa sababu hiyo isiyo na msingi, hili ni tatizo.
 
JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW

fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top