Na Sultani Kipingo Baada ya siku kadhaa za kupekua kila mahali kwenye vitabu vya historia, nimekuta hakuna ajuaye asili ya saluti. Ila nimekuta maelezo kwamba katika historia ya askari, mkono wa kuume (ama mkomo wa silaha) ulikuwa ukiinuliwa kama ishara ya salamu za kirafiki. 
Wanahistoria wanasema huenda hiyo ilikuwa ni ishara ya kuonesha kwamba hauko tayari kutumia silaha na kushambulia. Ila toka enzi hizo, ni askari asiye na cheo ama mwenye cheo kidogo ndiye alikuwa analazimika kutoa ishara hiyo mwanzo. 
Hadithi ingine ya kihistoria inatujuza  kwamba saluti hii ya askari ya leo imetoka enzi za Wafalme nchi za magharibi, ambapo askari aliinua mkono wa kuume na kugusa mfuniko katika kofia yake ya delaya kwa mbele ili afande apate kumjua wanapokaribiana. Hata hivyo, kitendo cha saluti ya askari imekuwa ya aina tofauti kwa karne na karne. Kuna wakati inasemekana ilikuwa ikipigwa kwa mikono yote miwili! Wakati mwingine saluti ilipigwa kwa mkono kuishia kifuani huku viwiko vikiangalia chini.
Hili linasemekana lilizuka katika meli za vita ambapo askari wa chini aghalabu huwa na mikono michafu kwa kazi za kusafisha meli, hivyo ilikuwa kama unamkosea adabu afande kumuonesha mkono uliojaa girisi. Pia kwenye makabrasha mengine ya kihistoria kumeonekana saluti za mkono wa kushoto.
Pia kuna maelezo ya kihistoria yanayosema kwamba ilikuwa ni kitendo cha lazima kwa askari wa cheo cha chini kuonesha heshima mbele ya afande wake kwa kuvua kofia, ambapo kiasi hili linaonekana lina ukweli fulani ndani yake. Hata hivyo saluti hii haikukaa sana kwani makofia mengine ya askari yalikuwa kazi kuyavua chap chap.
Hivyo kwenye karne ya 18 na 19, askari wakaachana na hiyo saluti ya kuvua kofia, na badala yake kukaja kugusa kofia hiyo kwa mbele. Baada ya hapo, staili zikabadilika badilika hadi hii saluti ya kisasa ikawa imeshika hatamu. Askari wa Ujerumani chini ya Adolf Hitler walikuwa na saluti ya aina yake toka achukue madaraka mwaka 1933, ile ya kunyoosha mkono mbele na iliitwa  "Hilter Salute"  ambapo si askari tu hata raia walitakiwa kuipiga huku wakimaka "Heil Hitler!"  Ila ikaja  kupigwa marufuku baaada ya Hitler kuangushwa mwaka 1945 katika vita kuu ya pili ya dunia.
Katika miaka ya 1745 (takriban karne mbili na nusu zilizopita) inasemekana katika kitabu cha kanuni za jeshi la uingereza kinasema: "Askari wanaamriwa kutovua kofia zao wanapopishana na afande, ama kusemeshwa naye, ila wanatakiwa kugusa paji la uso kwa vidole vya mkono wa kuume na kuinama wakati wa kupishana na afande"  Kwa vyovyote vile, kitendo cha mwenye cheo cha chini kumpigia saluti afande ni cha kuonesha heshima, na pia kutambua umuhimu, wajibu na ufahari wa kazi za uaskari.

JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW

FACEBOOK@EDONETZ  ,TWITER@EDONETZ INSTAGRAM@EDONETZ NA YOUTUBE@EDONETZ TV
 
Top