Inasemekana
kila jina lina asili yake na maana pia. Hata hilo jina lako ulipewa kwa sababu,
na lina asili yake. Kama si la kutoka katika Biblia ama Quran, basi ni la kimila
lenye kumaanisha jambo, kama vile siku, tukio, mahali ama hata shida au raha
aliyopata mama wakati wa uzazi wako.
Jiji la
Dar es salaam zamani liliitwa Mzizima. Sultani Seyyid
Majid wa Zanzibar ndiye aliyelipa jiji hili jina "Dar es
Salaam" linalotokana na lugha ya Kiarabu (Dār as-Salām) lenye
kumaanisha "nyumba ya amani." Maelezo yanayopatikana mara nyingi kuwa
maana ni "bandari ya salama" yachanganya maneno mawili yanayofanana
katika Kiarabu yaani "dar" (=nyumba) na "bandar"
(=bandari).
Dar es
Salaam ilichaguliwa na wakoloni Wajerumani kuwa mji
mkuu wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kwa sababu
ya bandari asilia yenye mdomo pana ya mto Kurasini. Kuanzia 1891
Dar es Salaam ilichukua nafasi ya Bagamoyo kama makao makuu ya
utawala. Bandari pamoja na ujenzi wa reli ya
kati kwenda Kigoma tangu 1904 ziliimarisha nafasi ya mji
ulioendelea kama mji mkuu baada ya Tanzania bara kuwa koloni ya Tanganyika chini
ya Uingereza.