Ni tuzo zinazosherehekewa zaidi kuliko zote barani Afrika. Ni
tuzo zenye heshima zaidi na maandalizi yake hujumuisha mbwembwe za kila aina.
MTV MAMA 2016, kwa mara nyingine tena inawakutanisha wababe wote
wa muziki barani Afrika kwenye jukwaa moja. Mwenyeji mwaka huu, ni jiji la
Johannesburg, jijini Afrika Kusini, likipokea kijiti kutoka kwa mji wa Durban
uliopata bahati ya kuziandaa kwa miaka miwili mfululizo.
Macho na masikio ya Waafrika wengi sasa yanaelekezwa huko na
kila nchi yenye wawakilishi ikiomba warudi na tuzo nyumbani waipe heshima nchi
yao.
Kizuri ni kwamba Ukitoa Afrika Kusini na Nigeria zenye wasanii
wengi zaidi waliotajwa kuwania, Tanzania nayo inashikilia nafasi ya juu kwa
uwakilishi. Diamond, Alikiba, Vanessa Mdee, Yamoto Band, Navy Kenzo na Raymond,
wameifanya Tanzania iwe na wawakilishi 6 mwaka huu – si haba na ni ishara kubwa
kuwa muziki wetu unazidi kuwa na nguvu.
Kama hiyo haitoshi, jukwaa la MAMAs litapandwa na wasanii wawili
wa Bongo Flava, Diamond na Alikiba, mahasimu wanaotengeneza pande mbili za
mashabiki wanaosigana kila leo. Uwepo wa wawili hao kwenye tuzo hizo mwaka huu
tena wakishare jukwaa moja, kunazifanya tuzo hizo mwaka huu ziwe za aina yake.
Kuna muitikio mkubwa pia wa wasanii wengine wa Tanzania katika
kuwaunga mkono wasanii wote waliotajwa mwaka huu. Yapo matarajio makubwa kuwa
huenda nusu ya wasanii hao waliotajwa mwaka huu, wanaweza kuja na ushindi
nyumbani. Kila lakheri kwa wote. Edonetz inawaombea ushindi wote watanzania katika kukuza mziki wa bongo,,,,,,,