Katika mfurulizo wa  makala ninazokuletea kila siku leo tuangalie ndoa na Ndoa itakuwa baraka pale wachumba wanapokuwa wamependana kwa dhati  na kwa hiari yao, pale wanapoona ni muda muafaka kuwa kitu kimoja kama mke na mume. Lakini kwa upande mwingine ndoa inakuwa ni balaa na kupoteza maana pale wachumba wanapoamua kuingia katika ndoa bila sababu za msingi wala vigezo vya maana kati yao. Basi kwa siku ya leo Hebu tupeane sababu mbovu kabisa ambazo kama utazitumia kama kigezo cha kufunga ndoa basi umeumia mwenyewe.
KUSEMA UMRI WANGU UNAZIDI KUWA MKUBWA
Hasa wanawake mara nyingi wanajitahidi kukimbizana na muda na wanaweka mkakati kabisa kwamba nikifikisha umri fulani lazima niwe ndani ya ndoa. Inawezekana unatumia kigezo cha kuwahi kabla hujapoteza muonekano lakini nakuambia wazi kabisa kama unaingia katika ndoa kwa sababu hii, andika maumivu siku zijazo.
Si kwamba usipoolewa basi wewe si mwanamke na kwamba ni mbaya, hapana ndoa ni taasisi ambayo si kila mtu amepewa uwezo wa kuwa mwanachama kwa hiyo ikija nafasi ya wewe kuwa mwanachama ingia bila matatizo lakini si kujidai unakimbizana na muda.
KWA PUPA YA MALI AU UTAJIRI WA MWANAUME/MWANAMKE
Kipindi cha nyuma jamii ilishazoea kwamba mwanamke kuolewa na mtu hata asiyempenda kwa kigezo cha mali za huyo jamaa ni kitu cha kawaida, lakini bwana siku hizi hadi wanaume nao kigezo hiki wanakitumia ili kutoka kimaisha. Na ombea huyo unayemdanganya asijue kabla hujafaidika kwani akijua atakuwahi na utakuwa umekosa ulichotaka. Wengi wao wanakumbana na mateso makubwa  wanapoingia katika ndoa kwa sababu ya mali za huyo mwenzake.
KUSHINDANA NA RAFIKI ZAKO
Sababu hii huwa ni asili kwani mara nyingi binadamu tumekuwa na hulka ya kujilinganisha na wenzetu. Sasa unapotaka kuingia katika ndoa kwa haraka kwa kuwa tu rafiki yako ameolewa juzi unajitia matatizoni mwenyewe. Wengi hupata ushawishi pale wanapohudhuria sherehe za harusi za ndugu na marafiki na shamra shamra za ukumbini kwa usiku huo zinawadanganya na kudhani hiyo ndio ndoa na huku kichwani akijenga wazo la yeye pia kutafuta mtu kwa haraka ili afanye kama mwenzake.
NJIA YA KUIMARISHA UHUSIANO
Wengi wanatumia sababu hii kulazimisha ndoa pale wanapoona mahusiano yao katika kipindi hicho sio mazuri sana kwa hiyo wanaona njia pekee ni kuingia katika ndoa haraka ili kubadilisha mazingira pengine mambo yatanyooka na kumtuliza mwenzake.
Kama utatumia sababu hii kujifunga kitanzi basi umeingia chaka kwani sio sababu ya msingi kukufanya ulazimishe ndoa. Kama katika kipindi hiki cha uchumba mnatofautiana si kwamba ndoa ndio itawafanya muwe na mtazamo mmoja kihisia na maamuzi.
KUTAKA MUWE KARIBU ZAIDI
Wachumba ambao wanaishi mbali mbali wanadhani kuingia katika ndoa haraka ni njia ya kumaliza umbali baina yao. Na maamuzi haya mtu anaweza kuyafanya hata kwa kuhama mji na kuhamia alipo mwenzake na kuanza kulazimisha ndoa hata kama mwenzake hajaonyesha utayari.
“Oh! nimechoka kuwasiliana naye kwenye simu kila siku bora nimfuate huko huko aliko na nimlazimishe anioe”. Kweli yawezekana unaumia lakini lazima uzingatie umbali wenu unaletwa na nini,  na ukishagundua shirikiana na huyo mwenzako namna ya kutatua ndio utajua kama na yeye yupo tayari na huo mpango wako au la na sio kumvamia alipo na kulazimisha mambo.
ILI UONDOKE KATIKA NYUMBA YA FAMILIA
Kama uliweza kulelewa hapo nyumbani kwenu kwa miaka mingi ndoa isiwe kigezo cha kukuondoa. Kweli kiumri umekua na unatamani uwe kwako ambako utakuwa una maamuzi ya leo unafanya nini au unapika nini. Na hapa inatokea mara nyingi pale msichana anapotembelea sehemu anayoishi mvulana na kukuta jamaa kiasi fulani kajipanga na anatamani ahamie hapo haraka kwa kumlazimisha ndoa,  kwani anaona kashapata njia ya mkato.

KISASI KWA ULIYEACHANA NAYE
Hapa napo wananasa wengi sana, yaani utakuta mtu anaachana na mchumba mwezi mmoja nyuma na kwa kuwa alimpenda na anataka kumlipizia kisasi basi analazimisha kuingia katika ndoa na mtu mwingine ambaye hajakaa naye hata mwaka kumfahamu.

JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top