Majumbani mwetu ni eneo muhimu sana kwetu, kwani kuna dhima nyingi sana ambazo zinakamilishwa majumbani mwetu katika kutufanya tuzidi kusonga mbele kimaisha. Kuna methali ambayo inasema, "Ngombe anapoumia malishoni hukimbilia zizini." Hii ina maana nyingi , lakini moja kwa moja inahusu nyumbani.

Tunaweza kupambana na kisirani kikubwa kwenye shughuli zetu za kila siku, tukajikuta tunalazimika kurejea nyumbani kwa ajili ya kupata amani. Kuna wakati majumbani mwetu kuna amani lakini jirani au jirani zetu ni kisirani kikubwa. Imeshatokea watu wakauza nyumba zao au kuhama nyumba walizopanga, kwa ajili ya kuwakimbia jirani wakorofi.

Jirani anaweza kuwa mkorofi kwa njia mbaimbali. Anaweza kuwa ni mwenye maneno yasiyoisha, anaweza kuwa mgomvi, anaweza kuwa mbea, anaweza kuwa mdokozi sana, anaweza kuwa ni mkosefu mkubwa wa adabu au vinginevyo.

Kuna wakati mimi mwenyewe nilikuwa na jirani ambao tulikuwa tunachangia nyumba. Kwa kweli, watu hawa, mtu na mumewe na watoto walikuwa ni walevi sana. Kila siku usiku na hata mchana walikuwa kwenye vita moja au nyingine. Kuna wakati tulikuwa tunashindwa hata kulala usikukucha.

Kwa kweli ningekuwa naweza kuhama ningehama haraka sana, lakini sikuwa na uwezo huo. Hivyo ilibidi nijitahidi kutafuta njia au mbinu ya kuishi. Ukweli ni kwamba niliweza kufanikiwa kwa mbinu hizo kumudu kuishi.

kwanza tunatakiwa kujua Kama una jirani mkorofi au kama utakuja kuwa na jirani mkorofi, naomba utumie mbinu hizi, kwani naamini zitakusaidia.
…Jambo la kwanza.., nililofanya ni kubainisha kile wanachofafanya, yaani ukorofi wao.
….Jambo la pili.., nikabainisha wakati ambapo wanafanya ukorofi huo,
…Jambo la tatu.., nikabainisha namna wanavyofanya. Niliandika kabisa kila kitu, kwa mfano muda gani wanafungua mziki kama vile kuna shereha, wakati gani na kwa namna gani wanapigana, ni nani na nani wanapigana zaidi na mengine.

Nilibaini kwenye baadhi ya vitendo vyao, yale ambayo ni kinyume na sheria za nchi na yale ambayo yanakera, lakini siyo kinyume na sheria. Nilibainisha hivyo ili kuona kama itanilazimu nisaidiwe na vyombo vya dola kutafuta suluhu.

Halafu nilirejea kwangu mwenyewe. Nilijiuliza kuhusu kama mimi mwenyewe huwa sivunji taratibu ambazo kwa kawaida zingepaswa kuwakera jirani zangu. Lakini, nilijiuliza kama siyo tu mazingira ya kazi yangu ndiyo chanzo cha kuona 
nakerwa?  Nilikuwa napenda sana kufanya kazi za kuandika usiku, kwani mchana nilikuwa nafanya kazi za uwandani zaidi(field)

Kwa mfano, mtu anaweza kudhani jirani zake wanamsumbua sana kwa sababu, amegeuza nyumbani kwake ni mahali kwa kusalia au kufanyia tahajudi. Hivyo kelele kidogo tu, anaweza kuhisi kwamba, anasumbuliwa sana.

Nilibaini kwamba, hata mimi sikuwa safi sana kama nilivyokuwa nafikiria. Nilibaini kwamba, kuna wakati nilikuwa najaza uchafu mahali ambapo tulikuwa tunatupa uchafu, halafu sishughuliki kujua nani ameutupa uchafu huo. Kumbe hawa jirani walikuwa wanafanya kazi hiyo. Hawakuwahi hata mara moja kulalamika.

Lakini niligundua pia kwamba, nilikuwa ninawashiti' waziwazi hawa jirani zangu na wakawa wanajua hilo. Hivyo kuna wakati walikuwa wanafanya visa vyao ili kunikera.
Nilikuwa sijaoa, hivyo nikija na msichana hapo nyumbani, kama wakiwepo, ilikuwa ni vurugu ya kufa na kupona. Ndilo nililogundua baaada ya kujiuliza maswali.

Nilichofanya ni kuanza kuwaonyesha kwamba, nawaheshimu, nikawa nawalipa watu kuja kuzoa zile taka na siku nyingine nikija na vitu nyumbani nawagawia kidogo. Nilishangaa kwamba, walianza kupunguza visa vyao.
Kwa mfano, hata wakiwa wamelewa na kuanza vurugu, nikitoka kuwachungulia kutokana na hali hiyo walikuwa wanapunguza kelele na walikuwa wakisema,  unaona fujo zako, hadi unamkera mtu asiyehusika.'

Nilizidi kuwafanyia kwa wema sana mambo mengi, bila kujigeuza b.w.#.g.e. Hatimaye niligundua kwamba jirani wengi huwa wanakera, wakati mwingine wakiwa hata hawajui kwamba, wanakera. Kuna wakati ujirani unakuwa mbaya kwa sababu, jirani wote ni wakorofi, hakuna aliyetayari kuwa na busara na kujishusha.

Kuna wakati hata hivyo unaweza kuwa mwema na ukajitahidi sana kuwafanya waone tatizo lao, lakini wakashindwa kuliona na kulikubali. Inapofikia hatua kama hiyo, inabidi kama nilivyosema awali uangalie kama jambo husika ni kinyume na sheria. Kama ni kinyume na sheria, inabidi uende kwenye vyombo vya sheria. Kama siyo kinyuime na sheria, inabidi bado uwe mpole na kutafuta mtu wa kati ambaye mtakaa naye na huyo jirani kujaribu kutafuta suluhu.

Ni vizuri kukagua kama maudhi ya jirani yanawakera jirani wengine. Kama yanawakera, kuna haja ya wewe kuanzisha umoja na hao jirani wengine, ambapo kwa pamoja mtakaa na kutazama namna ya kumsaidia au kumkabili jirani mkorofi na kumaliza kero zake. Kuna wakati jirani wengi wakiwa na kauli moja kuhusu kusumbuliwa na jirani, sheria inaweza kulitazama jambo hilo kwa makini.

Kama ni nyumba ya kupanga na jirani yako ni mpangaji mwenzako, ni vyema kumwona mwenye nyumba na kumweleza tatizo lako. Kuna uwezekano wa mwenye nyumba kuliona tatizo lako na kulielewa na hivyo kumpa notisi jirani huyo mkorofin ili ahame.

Nina uzoefu wa kutosha kwamba, mara nyingi vita ya majirani ni matokeo ya ujuaji wa majirani wote. Kama mmoja akiwa mwelewa, uwezekano wa kuyeyusha ukorofi wa mwingine ni mkubwa.
JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW

fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top