WASOMI huiita ‘thermos’. Watu wa kawaida huiita chupa ya chai.
Ni chupa maalumu ambayo hutumiwa kuwekea vitu vya joto, hususan chai na ikabakia ya moto kwa masaa kadhaa kabla haijapoteza joto na kuwa ya baridi. 
Vilevile chombo hiki kinaweza kutumiwa kuhifadhia vitu vya baridi na vikabakia katika hali ya ubaridi kwa masaa kadhaa kabla ya kupoteza hali hiyo.

*Alikuwa raia wa Scotland
*Aliivumbua mwaka 1892
Hata hivyo, kwa matumizi ya watu wa kawaida yaani ‘walalahoi’ chupa hiyo hutumiwa kuwekea chai tu. Hii ni pamoja na ukweli kwamba chombo chenyewe ni kidogo.

Kwa Kiingereza chombo hicho huitwa “vacuum flask”.  Kimeitwa hivyo kwavile huwa kina chupa  mbili ndani – moja kubwa ikiwa nje na ya pilindogoikiwa ndani – zikiwa zimetenganishwa na nafasi tupu lakini zikiwa zimeunganishwa pamoja kwenye shingo ambapo juu yake huwekwa kizibo.

Kujua hilo, ivunje chupa hiyo utagundua huwa kuna chupa nyingine ndogo ndani!

Iliitwa “vacuum flask” kwa vile eneo linalozitenganisha huwa limenyonywa hewa yote na kubakia halina kitu, hiyo ndiyo maana ya neno ‘vacuum’, yaani sehemu iliyo ‘tupu’ au  au ‘sehemu isiyokuwa na hewa’.Fahamu kwamba hewa ndiyo kitu kikubwa katika kupoza au kuhifadhi joto au baridi.

Ukiitoa thermos kwenye ganda lake la nje na kuitazama chupa ya ndani utaona chupa hiyo ina kimkia kilichotokeza chini yake.

Hiyo ni ncha iliyotumika kunyonya hewa ya ndani kati ya chupa mbili na kuiziba sehemu hiyo isiingie tena hewa.  Kimkia hicho kikivunjika, hewa huingia katikati ya chupa husika mbili na kuifanya isiweze kutunza tena hali ya joto au baridi ya kitu kilicho ndani.

Chombo hicho maarufu duniani, kwa matajiri walioko jijini London na kwa maskini walioko, Nzega, Lushoto na Mwananyamala, kiligunduliwa na raia mmoja wa Scotland, Uingereza, aliyekuwa mtaalamu wa fizikia na kemia, Sir James Dewar (pichani)mwaka 1892.  Chombo hicho pia hujulikana kama ‘Dewar flask’ likiwa ni jina la mvumbuzi wake.

Thermos za mwanzo kibiashara zilitengenezwa mwaka 1904 na Kampuni ya Ujerumani iliyojulikana kama Thermos GmbH ambapo chupa hizo ziliitwa thermos, neno ambalo sehemu nyingi duniani limebakia kuwa kielelezo cha chupa zote za aina hiyo.

Ndiyo maana chupa hiyo watu wengi huiita thermos.
Kwa ujumla chupa hizo hutengenezwa kwa kutumia chuma, kioo, sponji, plastiki na kadhalika, ili kulinda joto au baridi inayotakiwa ndani yake. 

Pia kuna matumizi ya vitu au madini yenye kuweza kuakisi mwanga au mionzi kwenye chupa hiyo ambapo Dewar alitumia madini ya fedha (silver).

Chupa hiyo inaweza kuweka kitu cha baridi na kikaendelea kuwa hivyo kwa saa 24, na cha moto kikaendelea katika hali hiyo kwa saa nane.

Katika maabara na viwandani, chupa hizo hutumia kutunzia vitu vya majimaji ambavyo baadaye hugeuka kuwa gesi, kama vile ‘Oxygen na Nitrogen’. 

Hata hivyo, chupa hizo huwa zina vizibo maalumu vya kutolea hewa nje kidogo ili kuzuia kujaa kwa gesi katika chupa na kuifanya ipasuke.

Huo ndiyo uvumbuzi wa Sir James Dewar aliyezaliwa Septemba 20, 1842 na kufariki Machi 27, 1923 akiwa na umri wa miaka 80.
Ni uvumbuzi ambao hata Wazaramo wa Kisarawe na Wasukuma wa Sengerema wanauona na kuutumia


 
Top