UCHUNGUZI unaonesha
kuwa kila mtu anapenda kujitegemea, lakini wengi wanashindwa kufanya hivyo kwa
sababu ya kukosa kitu wanachokiamini, nacho ni kutokuwa na uwezo wa kufanya
hivyo!
unapowauliza kwa nini
wanazeekea kwenye maisha ya utegemezi. Sababu ya kukosa uwezo imewafanya baadhi
ya watu kuwa tayari kupokea kila aina ya manyanyaso na mwisho wa yote
wanajipoza kwa kulia.
Swali la kujiuliza: Ni nani aliyezaliwa
anajitegemea? Jibu ni HAKUNA, kupitia
vipengele vifuatavyo msomaji utajifunza jinsi ya kuanza maisha ya kujitegemea.
1.
MTAZAMO
Kikwazo cha kwanza
kinachowafanya watu waishi maisha ya utegemezi ni mtazamo. Wengi wanaamini wana haki ya kulelewa na
wazazi/ndugu, lakini wanashindwa kujiuliza wataishi katika utegemezi mpaka lini
na wanaowategemea wakifariki dunia wataishije?
Kazi ya kwanza katika
kuyaelekea maisha ya kujitegemea ni kubadili mtazamo wa maisha tegemezi na
kuona umuhimu wa kujitegemea. Maana yangu hapa ni kuyachukia maisha ya
kumtegemea mtu na kutamani maisha ya kujitegemea ambayo ni huru na yenye raha.
2.
JITEGEMEE
NDANI YA UTEGEMEZI
Baada ya kubadilisha
mtazamo, mhusika ni lazima aanze maisha ya kujitegemea ndani ya utegemezi.
Msingi wa kipengele hiki ni huu; kuna baadhi ya watu wanabweteka mno na kutaka
wafanyiwe kila kitu na walezi wao ambapo hata andazi la shilingi 100 wanataka
wanunuliwe! Kisingingizio ni kilekile, kwamba hawana uwezo ingawa fedha kama
shilingi mia mbili wanazipata.
Kujifunza kujitegemea
lazima kuanzie ndani ya maisha ya kutegemea, mfano kama jukumu la baba ni
kununua mboga na wewe umebahatika kupata kiasi cha fedha kwa njia yoyote hata
ya kupewa, usizifiche, badala yake lichukue jukumu la baba na kulifanya
wewe. Tabia hii inajenga msingi wa uwajibikaji ambao ndiyo nguzo ya maisha
ya kujitegemea.
Chukia maisha ya
kufanyiwa kila kitu, jihangaishe kwa kazi ya aina yoyote, jiwekee utaratibu wa
kuhudumia familia yako, weka msingi wa kuheshimu fedha, usiendekeze tabia ya
kupata fedha na kuacha kufanya jambo la maana nyumbani kisa unamtegemea mtu
atakununulia hiki na kile na kuzifanya fedha zako ziwe za kutapanya ovyo.
Ukijizoeza hivyo hutaweza kujitegemea.
Kwa leo naomba niishie
hapa, ila nikuache na swali hili:
Ni mara ngapi umekuwa
ukimsaidia mlezi wako kukabiliana na changamoto za kuendesha maisha? Kama unafanya hivyo tambua umeanza mazoezi ya
kujitegemea, endelea kufanya hivyo lakini kama umebweteka tu nyumbani tambua
uzee utakukuta ukiwa mtumwa wa mtu.
3.
JIAMINI
Vikwazo au shaka
juu ya kuweza kumudu maisha ya kujitegemea vimewafanya wengi wasijiamini. “Kwa
kipato hiki nitaweza kweli kuendesha maisha yangu, nilipe kodi ya nyumba,
chakula, mavazi na mahitaji mengine?” Maswali ya aina hii mara nyingi yamekuwa
na majibu ya haitawezekana!
Tabia ya akili hasa
katika kufikiria mambo yajayo ni kujenga hofu ambayo wakati mwingine
haihitajiki; wenye kujiamini pekee ndiyo ambao hutupilia mbali hofu na
kujiamini ndiyo walioofanikiwa katika maisha yao.
Kwa msingi huo,
unapofikiria maisha ya kujitegemea usiwaze sana juu ya kuwezekana kwa mambo,
jiamini kuwa utaweza, ukifanya hivyo utaweza; siku zote mwenye shaka havuki
mto!
4.
CHUKUA
HATUA
Hatua nyingine muhimu
baada ya kupita vipengele nilivyoanisha hapo juu ni hiki cha kuchukua hatua.
Watu wengi wamekuwa wakipanga kujitegeme, lakini kila mwaka wanaahilisha
kufanya hivyo. “Nafikiri nitahama mwaka ujao.” Mwaka ukifika anapanga kufanya
hivyo mwaka unaofuata matokeo yake anazeeka akiwa kwenye maisha tegemezi.
Ushauri wangu, baada
ya kujiamini kuwa unaweza chukua hatua ya kutoka mahali ulipo, jambo kubwa la
kuzingatia hapa ni kuhakikisha kuwa uchukuaji hatua lazima uambatane na ushauri
mzuri kutoka kwa ndugu na jamaa na hasa wale uliokuwa unaishi nao kama
wanakuunga mkono katika suala hilo.
5.
USIRUDI
NYUMA
Uchunguzi unaonesha
kuwa wapo watu ambao hupitia hatua zote za kuelekea kujitegemea, lakini
wanapozikabili changamoto za maisha hayo huamua kurudi mahali wapokuwa wanaishi
jambo ambalo huwaongezea fedheha na mara nyingine kuwaathiri kisaikolojia.
Unapokuwa umeanza
maisha ya kujitegemea suala la kurudi ulipotoka lisiwe la kawaida. Kumbuka
unapokuwa na wazo la “nikishindwa narudi kwa baba,” huwezi kujituma,
hutapambana na changamoto za maisha binafsi kwa vile kinga yako haitakuwa kwako
bali kule ulikotoka, kushindwa itakuwa ni sehemu yako.
6.
ONGEZA
MARAFIKI
Unapokuwa kwenye
maisha ya kujitegemea hakikisha kuwa unajitahidi kupunguza maadui. Fanya kila
linalowezekana kuongeza marafiki ambao siku zote ndiyo nguzo muhimu nyakati za
shida. Kumbuka kazi ya rafiki ni kufariji na adui kuangamiza!
Baada ya kusema hayo,
naamini mada hii itawasaidia wengi, furaha yangu ni kusikia baada miezi, miaka
michache kuwa watu wengi walijitegemea kutokana na hamasa waliyoipata kwenye
soma hili!
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv