WANJA ni moja ya kipodozi muhimu kufanya macho yavutie na kuongeza mvuto na muonekano wa sura yako. Watumiaji wa wanja wanalijua hilo.
Siku hizi wanja unatengenezwa katika aina tatu, pensili, wa maji (liquid) na wanja wa gel/cream. Pia zinakuja katika rangi aina mbalimbali hivyo una uhuru mkubwa wa kuchagua aina na rangi unayotaka. Ila kuna vitu vichache vya kuzingatia;
Paka wanja baada ya kupaka foundation au poda (facial powder) kwenye uso wako, maana ukianza kupaka wanja kisha upake poda utavuruga wanja uliopaka kwenye nyusi.
Chana nyusi kwa kitana chenye meno madogo kabla ya kupaka wanja, itasaidia kuzifanya nyusi zinyooke na kukaa katika mstari na itakuwa rahisi kwako kupaka wanja.
Chagua wanja utakaoendana na rangi ya nywele zako iwe umesuka rasta, umevaa wigi, nywele ‘natural’ na kadhalika, muhimu chagua rangi ya wanja itakayoendana na nywele zilizopo kichwani mwako, kama ni nyeusi, kahawia, damu ya mzee nk.
Ukiwa unaenda kazini au ofisini paka wanja kidogo, usikoleze sana ila kama ni mitoko mingine unaweza kuukoleza upendavyo. Pia kwa ofisini rangi nzuri ya kupaka wanja ni nyeusi na kahawia, ila rangi nyingine yoyote unaweza kupaka kwenye mitoko mingine kama harusi, matembezi ya jioni na mengine.
Ukinyoa nyusi ni rahisi kupaka wanja na utavutia zaidi, ila hakikisha unanyoa nyusi kwa watu wazoefu ili wakunyoe kuendana na nyusi na sura yako ilivyo hata ukipaka wanja utapendeza. Ukitaka nyusi zinyooke vizuri paka vaseline kidogo kisha paka wanja na utakaa kwa muda mrefu.
Kwa mtu unayeanza kujifunza kupaka wanja, anza kutumia wa pensili maana ni rahisi kupaka, wanja wa maji na gel unahitaji uzoefu.
Chonga wanja wako kwa vichongeo vya pensili usitumie viwembe vilivyotumika kuchongea wanja vinaweza kuleta vijidudu kwenye wanja.
Wanja wako kabla ya kupaka hakikisha umechongwa vizuri ili uweze kupaka mara moja bila kurudia rudia sana kama haujachongwa vizuri, sehemu nyingine utakolea sana sehemu nyingine itakuwa hafifu na haitapendeza.
Haya mashosti mambo ya wanja hayo msije kusema hamjui mbinu na ujanja wa kupaka wanja.


JIUNGE NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz  , twiter@edonetz  , inst@edonetz_blog  na  youtube@edone tv
 
Top