Sio kitu kibaya kujuliana hali na kutambulisha mambo ya
msingi yanayoendelea katika mahusiano yako wewe na mpenzi wako kwa marafiki
wa karibu au ndugu na jamaa kufahamu kushirikiana nanyi katika mapenzi
yenu kama vile wakati wa sherehe au msiba.
Lakini kuna wakati watu wengine wa pembeni, wawe majirani,
ndugu, wazazi au marafiki wanaweza kuwa wabaya au sumu ya mahusiano yako,
hasa pale mnapotegemewa sana kutoa msaada, maoni au maelekezo katika
maisha yako
Unaweza kufanya yafuatayo yatakusaidia sana.
Udhibiti wa taarifa kwa wengine:
Kadri unavyoelezea mahusiano yako kwa watu wengine ndivyo
unavyowapa nafasi watu kutoa maoni, na hata kudhani kuwa wana dhamana ya
kukuelekeza unavyotakiwa kuishi na mwenza wako. Hivyo basi, chukua muda wa
kutosha kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu masuala yako ya mahusiano
kabla hajaanza kutafuta maoni, ushauri kwa watu wengine.
Upekee wa mambo:
Tambua kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya
kipekee, mazingira pia ya tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa
wengine yanaweza kuwa ni ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza
yasikusaidie moja kwa moja katika suluhisho lako.
Mwenye maamuzi ni wewe:
Ni kweli kuwa kuna nyakati ni muhimu kupata ushauri kutoka
kwa watu wengine, na zaidi sana watu wenye uelewa sahihi na unaowaamini,
hakikisha kuwa unatambua kuwa wewe mwenyewe ndio mwenye kubeba lawama ya
maamuzi utakayochukua.
Kuwa na subira:
Usichukue maamuzi ya haraka katika mahusiano hususani
uamuzi wa kuamua kuwashirikisha watu wengine habari ya mambo yahusuyo
uhusiano wako. Unapofanya uamuzi wa kuwashirikisha wengine kwa
haraka unajinyima nafasi ya kulichunguza jambo kwa ufasaha hususani madhara
yanayoweza kutokea kwa kuwaeleza wengine, au kama ni tatizo, basi
kufikiria njia sahihi ambazo ungeweza kuzitumia kupata suluhu ya
tatizo.
Fungua njia za mawasiliano kati yenu:
Pengine chanzo cha wewe kutaka kuzungumza mambo ya ndani
yanayohusu mahusiano yenu kwa watu wengine ni kwa kuwa umekosa
nafasi ya kuzungumza kwa ufasaha na mwenzi wako. Tafuteni nafasi za
kutosha, jengeni mazingira ya kuzungumzia mambo yenu kabla ya kutaka
kuwashirikisha watu wengine.
Kuweni peke yenu:
Hata kama hautaki kueleza watu kuhusu mambo yanayoendana na
maisha yenu, mazingira unamoishi yanaweza kuchangia watu kutaka
kuingilia mahusiano yenu kwa kutoa maelekezo, ushauri au maoni kuhusu
muishivyo wewe na mpenzi wako. Inapobidi hakikisha hamuishi karibu na
wazazi wenu, ndugu au rafiki wa karibu.
Jifunze zaidi :
Kumbuka mahusiano yanahitaji sana uelewa mkubwa wa jinsi ya
kufanya mawasiliano fasaha, kuelewa hisia za mwenzi wako, kutambua mbinu
za kusuluhisha migogoro na zaidi sana kufanya mipango ya muda mrefu ya
uhusiano wenu. Jizoeshe kusoma makala na vitabu mbalimbali vyenye
kuboresha ufahamu wa mambo ya msingi.
JIUNGE
NASI KWA KUTUFOLLOW
fb@edonetz , twiter@edonetz , inst@edonetz_blog na youtube@edone tv